UWT watoa msaada wa Sh7 milioni Mwananyamala

Muktasari:

  • “Tumependelea siku hii iwe maalumu kwa ajili ya kutembelea wenzetu waliopo hapa ili wafurahi na ndiyo maana msaada huu umelenga wanawake wenzetu,” amesema Mwaikambo

Dar es Salaam. Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi wameadhimisha siku ya mwanamke kwa kutoa msaada kwa akina mama katika Hopitali ya Mwananyamala wilayani Kinondoni yenye thamani ya Sh7 milioni.

Wametoa msaada huo leo Machi 8 ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Msaada huo ni pamoja na sabuni, taulo za watoto (pampasi), mabeseni, mafagio, dawa za meno ambavyo wamevikabidhi katika wodi za akinamama

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, katibu wa UWT Kinondoni, Nuru Mwaibako amesema mwanamke ni nguzo muhimu katika familia hivyo wanahitaji kuthaminiwa.

Amesema lengo la msaada huo ni kuwafariji akina mama hao kama sehemu ya kujumuika nao kuadhimisha siku hiyo.

“Siku ya leo ni maalumu kwetu sisi wanawake, hivyo tumeamua kuja kwa wenzetu hapa hospitali kama sehemu ya kuwatembelea wajione nao ni miongoni mwa wanawake duniani katika kuadhimisha siku hii muhimu,” amesema.

Mbali na sehemu hiyo ya msaada, Mwaibako amesema mwanamke ni mlezi katika familia, hivyo ameshauri wanawake wapewe heshima na kwa wale wanaowanyanyasa wachukuliwe hatua.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, mkazi wa Kinondoni Khairath Hamisi ameshukuru umoja huo kwa msaada waliowapatia na ameomba misaada hiyo iwe endelevu.

“Tunashukuru sana tumeletewa sabuni, pampasi na vingine vingi msaada huu utatusaidia kwa sababu pengine kuna watu hawakuwa na uwezo wa kuvinunua,”amesema.

Mwenyekiti wa umoja huo, Renalda Kageuka amesema lengo la msaada huo ni kuwafariji wanawake waliolazwa hospitalini hapo kwa matatizo mbalimbali.

“Tumependelea siku hii iwe maalumu kwa ajili ya kutembelea wenzetu waliopo hapa ili wafurahi na ndio maana msaada huu umelenga wanawake wenzetu,”amesema.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magojwa ya akina mama, Luzango Maembe amesema, “tunashukuru kupokea misaada hii kusaidia akina mama ambao wamekuja hapa kupata huduma.”