Uhaba wa maji unavyotishia afya za wanafunzi wa Ikolo

Muktasari:

Safari hii ilijumuisha wadau kutoka mashirika na asasi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya elimu ikiwa ni maadhimisho ya juma la elimu kimataifa (Gawe) ambayo kwa mwaka huu yalifanyika wilayani Mkalama mkoani Singida.

Baada ya kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 60 kutoka yalipo makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Mkalama hatimaye tunatia nanga katika kijiji cha Ikolo.

Safari hii ilijumuisha wadau kutoka mashirika na asasi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya elimu ikiwa ni maadhimisho ya juma la elimu kimataifa (Gawe) ambayo kwa mwaka huu yalifanyika wilayani Mkalama mkoani Singida.

Ugeni unapokelewa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Ikolo ambao licha ya sare zao chakavu nyuso zao zilionyesha dhahiri kutawaliwa na furaha.

Bila kujali miguuni hawana viatu imara wanafunzi hao wanazunguka uwanja wakiimba nyimbo ikiwa ni ishara ya kuwakaribisha wageni waliofika kuwatembelea na kufurahia ujio huo.

Mwalimu Mkuu wa Shule Ikolo, Elibariki Haule anawakaribisha wageni na kueleza mambo kadhaa kuhusu shule hiyo iliyoanzishwa miaka 46 iliyopita.

Kwa Haule kilio chake kikubwa ni upungufu wa madarasa, madawati, matundu ya vyoo, uhaba wa maji na uchache wa nyumba za walimu.

Wakati Haule akiendelea navutiwa na kundi la wanafunzi lililokuwa limejitenga pembeni. Wanafunzi hao walikuwa wakimshambulia mwenzao mmoja wakidai kuwa ananuka.

Nilipotaka kujua nini hasa chanzo cha mabishano ndipo nilipobaini kuwa uhaba wa maji katika kijiji ni mkubwa kiasi cha kuwafanya watoto kujisaidia bila kunawa.

Suala la kujisafisha na maji baada ya kujisaidia na kunawa mikono kwa sabuni mara baada ya kutoka chooni halipo kabisa vichwani mwa wanafunzi wa Ikolo.

Kuthibitisha hilo nazunguka upande ambao kuna jengo linalotumika kama vyoo na kukutana na watoto wanaoingia na kutoka bila kunawa mikono.

engo hilo la matofali ya kuchoma lina matundu manane yaliyochimbwa kienyeji lakini linahudumia jumla ya wanafunzi 581 wa shule hiyo ambao kati yao 491 wa darasa la kwanza hadi la saba na 90 wa darasa la awali.

Jackson Joseph ni mwanafunzi wa darasa la tano shuleni hapo anaeleza kuwa huwa hawatumii maji badala yake wanatumia makaratasi, majani au vitambaa kujifutia.

“Nikienda chooni najisaidia kisha najifuta kwa kitambaa au karatasi halafu nalitupa kwenye shimo, wengine wanatumia majani ila wapo pia ambao hawanawi, akimaliza anavaa nguo zake kisha anaondoka,”anasema Joseph

Joseph na watoto wengine shuleni hapo hawatambui kuwa wanaweza kupata magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuharisha kutokana na kutozingatia kanuni za usafi ikiwa ni pamoja na kubeba vijidudu kutoka chooni na kuviingiza tumboni kwa sababu ya kushindwa kunawa.

Hali hiyo inanisukuma kuzunguka huku na kule ili kujua ukubwa wa tatizo ndipo ninapobaini kuwa kuna uhaba mkubwa wa maji katika kijiji cha Ikolo na maeneo yanayokizunguka kijiji hicho.

Kutoka yanapopatikana maji hadi shuleni hapo ni umbali wa zaidi ya kilomita tatu.

Kufuatia hali hiyo walimu wa Ikolo wameweka utaratibu unaomtaka kila mwanafunzi kwenda shuleni akiwa amebeba kidumu cha maji cha lita tano.

Mwanafunzi wa darasa la sita, Juma Paul anasema utaratibu wa wanafunzi kubeba maji ni jambo la lazima shuleni hapo na mwanafunzi anaposhindwa kutekeleza agizo hilo anakumbana na adhabu ya bakora.

Cha ajabu ni kwamba maji hayo si kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi au shule bali yanakwenda kutumika kwenye nyumba za walimu.

Mwalimu Yohana Boay anathibitisha hilo na kueleza kuwa hawana namna ya kufanya zaidi ya kuwaagiza wanafunzi wabebe maji kutoka nyumbani.

Anasema ni changamoto ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu hivyo walimu wanalizimika kuwaagiza wanafunzi wabebe maji ili kunusuru muda wa vipindi kutumika kutafuta huduma hiyo ambayo ni muhimu kwa matumizi ya kila nyumba.

“Ni kweli hapa shuleni hakuna maji, na si hapa tu bali kijiji kizima kuna tatizo hilo, ndiyo sababu tunawaambia walete maji kutoka nyumbani. Mwalimu wa zamu ndiye mwenye jukumu la kugawa maji hayo kwa walimu wengine,” anasema Boay.

Boay anafafanua kuwa sababu ya kufanya hivyo ni kuwaondolea walimu adha ya kupoteza muda wa kufundisha kwa kwa ajili ya kwenda kutafuta maji.

“Haiwezekani mwalimu aache kufundisha darasani atembee umbali mrefu kutafuta maji kwa hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa basi tunaagiza waje na kiasi hicho kidogo cha maji na wakati mwingine wazazi wanawazuia.”

Kuhusu wanafunzi kutotumia maji vyooni Boay ambaye pia ni mwalimu wa afya shuleni hapo anakiri kufahamu ukweli kwamba wanafunzi wake wanajifuta kwa makaratasi na vitambaa.

Mwalimu huyo anafahamu pia kuwa hali hiyo ni hatari kwa afya za watoto lakini anadai hana namna ya kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuwa ni jambo ambalo lipo nje ya uwezo wake.

“Nikiwa ndiye mwalimu wa afya kwangu nazingatia usafi lakini inapofika kwenye suala la maji linakuwa nje ya uwezo wangu ila natambua kuwa watoto hawatumii maji chooni na hata sasa ukienda kwenye vyoo huwezi kukuta ndoo ya maji.”

Ofisa elimu msingi wa wilaya ya Mkalama, Chacha Kehogo anakiri kuwepo kwa changamoto ya maji katika kijiji hicho lakini hafahamu kama walimu wanawatuma wanafunzi kuwachotea maji ya matumizi yao.

“Si vibaya wanafunzi kuwasaidia walimu wao ila ilitakiwa wazazi ndio wafikie makubaliano hayo na kuona ni namna gani sahihi ya kuwasaidia walimu si kwa kuwatembeza watoto umbali mrefu na mzigo wa maji.”

“Nilikuwa sifahamu hilo suala ila nitalifuatilia na kutoa maelekezo kwa walimu watafute njia nyingine na hii sio kwa Ikolo tu bali walimu wa wilaya nzima,” anasema.

Diwani wa kata ya Mwangeza, Geofrey Msengi anasema kwamba changamoto ya uhaba wa maji inakwenda kupatiwa ufumbuzi hivi karibuni baada ya kutokea wafadhili waliojitolea kuweka mtandao wa maji katika eneo hilo.

“Kwanza nilikuwa sifahamu kama wanafunzi wamefikia hatua ya kujisafisha kwa kutumia vitu vigumu kutokana na kukosekana wa maji ila ninafahamu kuwa kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji eneo hilo,” anasema Msengi.

“Tukishapata maji hilo tatizo itakuwa mwisho na wafadhili wameshakubali kutusaidia kwa gharama yoyote ile tunachosubiri sasa ni utekelezaji wa mpango huo,” anasema Msengi ingawa hakuwataja jina wafadhili hao.