Uharibifu wa mazingira unavyorudisha nyuma vita ya kupunguza uhaba wa maji nchini

Muktasari:

  • Uhaba huo wa maji, mbali na kuathiri maisha ya wakazi husika kwa kuleta kiu, pia upo hatarini kuongeza migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambao kwa kiwango kikubwa hutumia maji kwa ajili ya kilimo na unyeshwaji wa mifugo.

Kuna kila dalili kuwa baadhi ya wanavijijini huenda wakaendelea kukumbana na uhaba wa maji safi na salama iwapo uharibifu wa mazingira karibu na vyanzo muhimu vya maji hautadhibitiwa ipasavyo.

Uhaba huo wa maji, mbali na kuathiri maisha ya wakazi husika kwa kuleta kiu, pia upo hatarini kuongeza migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambao kwa kiwango kikubwa hutumia maji kwa ajili ya kilimo na unyeshwaji wa mifugo.

Uchunguzi wa Mwananchi katika baadhi ya vijiji vya kata za Lionja na Namikango wilayani Nachingwea mkoani Linda umebaini kuwa mbali na wakazi wa maeneo hayo kukumbwa na uhaba wa maji safi na salama bado wanafanya shughuli za kiuchumi ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo muhimu vya maji.

Shughuli hizo zinafanywa licha ya kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kuzuia ujenzi wa makazi au shughuli zozote za kiuchumi ndani ya mita 60 zitakazohatarisha vyanzo vya maji ikiwemo mito, mabwawa, fukwe na bahari.

Sehemu kubwa ya wananchi wa vijiji hivyo vya Namikango A, Namikango B, Nangunde, Lionja A, Lionja B, Litandamtama na Nyambi B wanategemea maji yasiyo safi na salama yatokanayo na chemchemi na visima vifupi vya msimu kutokana na kukosa vyanzo vya uhakika kama mito na maziwa.

Hata hivyo, katika vyanzo vichache vya maji walivyonavyo baadhi ya wakazi hao wanaendelea na kulima mashamba yaliyokaribu na visima, wanafyatua tofali na kukata miti.

Katika kisima cha Chengo kilichopo katika kijiji cha Lionja A, kinachotoa huduma za maji yasiyo na chumvi misimu yote, mita tano kulia kuna shamba la vitunguu na upande wa kushoto kuna shamba la miwa.

Kisima hicho maarufu maeneo hayo kama “Kisima Mama” kinahudumia zaidi ya vijiji vinane vya Lionja A, Lionja B, Nangunde, Namikango A, Namikango B, Litandamtama, Naulingo na Lionja B, wakati wa kiangazi kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Lionja, Joachim Mnungu.

“Ni eneo la urithi ambalo familia yetu imelikuta na huwa tunalilima kila mwaka sioni sababu ya kuliacha,” anasema mmoja ya wakulima wa bustani jirani na kisima cha Chengo aliyekataa jina lake kuandikwa gazetini.

Alipoulizwa iwapo haoni ataathiri kisima hicho muhimu kwa uhai wa wakazi wa vijiji hivyo akiwemo yeye, alijibu; “lakini sichafui maji nachota na kifaa safi kama wengine wanaochota maji ya kunywa na kutumia nyumbani.”

Visima vingine vifupi vya udongo kama vya Litandamtama navyo vimezungukwa na mashamba ya korosho hadi mita mbili karibu navyo. Baadhi ya wakazi wanafyatua tofali na kuzichomea katika maeneo yenye asili ya chemchemi.

Katika Mto Mbwemkuru unaopita zaidi ya kilomita 10 kutoka kijiji cha Lionja nao pembeni wakulima wanaendeleza kilimo cha bustani licha ya kuwa ni moja ya chanzo muhimu cha maji wakati wa kiangazi na masika.

Wakazi wengine wanaotumia visima hivyo wanaeleza kuwa huwa wanawashauri wenzao kuacha shughuli katika vyanzo hivyo lakini imekuwa ni vigumu kwa kuwa hawana mamlaka ya kuwaondoa.

“Hatuwezi kumkataza mtu kulima kwa sababu ni shamba lake na hata ukimwambia hataki kuacha kulilima. Wapo wengi tu wanalima kila mwaka,” anasema Khadija Amour.

Pamoja na kuwa baadhi wanaendelea kulima katika maeneo hayo hususan kando ya Mto Mbwemkuru, Abass anasema wengi wanakula hasara kwa sababu mafuriko yakija huwa yanasoma kila kitu na kuwaacha tena “maskini”.

Baadhi ya wananchi wanahofu kuwa iwapo wenzao hawatadhibitiwa kuharibu mazingira karibu na vyanzo vya maji, hali itakuwa ngumu zaidi ya sasa.

“Hakuna vikao vya kuangalia usalama wa visima vyetu au utunzaji wa vyanzo vya maji. Nakumbuka katikati ya miaka 1980, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliagiza tupande miti karibu na kisima cha njia panda lakini hadi leo hapajapandwa miti,” anasema Shaban Majonjo maarufu kama Mzee Mkorosho, mkazi wa Kijiji cha Lionja A.

 

Viongozi wa vijiji na kata wanakiri kuwa uharibifu wa mazingira ndani ya mita 60 karibu na vyanzo vya maji unazidi kuyaweka maeneo yao katika sintofahamu ya uhakika wa maji miaka ijayo japo wanapambana na wahalifu hao.

“Hali inazidi kuwa ngumu zaidi sasa kwa sababu watu wanaharibu vyanzo vya maji. Tulikuwa na kisima cha ringi lakini tayari kimeshakauka kwa sababu watu walikuwa wanalima na wanakata miti katika eneo hilo,” anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Litandamtama, Bakar Libea.

Baada ya kisima hicho cha ringi kukauka, sasa wanakijiji wanalazimika kutembea kilomita moja kwenda kwenye kisima cha chumvi kilichopo jirani au kwenda Kijiji cha Lionja A kilichopo kilomita zaidi ya nne.

Libea anasema hata Mto Mbwemkuru unazidi kukauka wakati wa kiangazi sababu wakulima wamekata mashamba hadi ndani ya mto jambo lililofanya hata madimbwi yaliyokuwepo hivi karibuni kupungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo kipindi chote maji yalikuwa yanatiririka na kuwezesha uvuvi.

Kuhusu hatua wanazochukua kukabiliana na hali hiyo, Libea anasema wameunda kikosi kazi cha kukamata wote wanaofanya shughuli hizo kinyume na sheria na mwanzoni mwa mwaka huu wameshapanda miti 400 kwenye maeneo oevu na inaendelea vizuri.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wanaoharibu mazingira bado hawajakamatwa licha ya sheria ya mazingira kutaka kuadhibiwa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Namikango, Bakir Ngawanje anasema hadi mwanzoni mwa Agosti mwaka huu walikuwa hawajakamata mtu yeyote ila wanachofanya kwa sasa ni kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutunza mazingira kuepuka ukame siku zijazo.

“Sehemu za mabondeni wengi wanasema ni mashamba yao lakini tumeona hatuwezi kuwavumilia na sababu hizo. Tumewapa muda miaka miwili kuanzia mwaka jana watafute maeneo mengine ya kulima,” anasema.

Wadau wa uhifadhi wa mazingira wanasema uhaba wa maji utaongezekana miaka ijayo iwapo waharibifu wa mazingira hautadhibitiwa kwa sasa.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Uhifadhi wa Serengeti, Meyasi Meshilieck anasema vyanzo vya maji ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu, wanyama, ndege na mimea hivyo vikipotea maisha ya viumbe vyote hivyo nayo yatatoweka.

“Lazina sheria zinazolinda vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla zitekelezwe kikamilifu kuokoa maisha ya vizazi vijavyo. Kuna maofisa lukuki kuanzia ngazi ya kijiji hadi wizarani wanafanya nini?” anasema.

Anasema njia endelevu ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira yanayowazunguka kwa kupanda miti karibu na vyanzo vya maji na kuepuka shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo hayo.

“Wananchi wanaodai wakilima kwenye vyanzo vya maji wanapata kipato wanaweza kupata fedha nyingi iwapo watapanda miti mingi na kufanya ufugaji wa nyuki katika maeneo hayo hayo. Serikali ishirikiane kikamilifu na asasi za kiraia zinazoshughulikia uhifadhi wa mazingira kutoa elimu kwa wananchi kuhusu njia bora kama hizi,” anasema.

Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea unasema kuwa wameshapeleka barua kwa viongozi wote wa chini kupiga marufuku kulima au kufanya shughuli yeyote ndani ya mita 60 katika vyanzo vya maji.

“Wengi wamekubali wakiwemo wakazi wa kata ya Nditi na wale ambao hawaelewi bado tunaendelea kuwaelimisha umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji. Tulipanga kuwaondoa kwa nguvu ila wametuomba tuwape muda wavune mazao yao na baadaye wataondoka,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Arbogast Kiwale.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, anasema kuna sheria kuu na ndogo ndogo za utunzaji mazingira zinazohitaji kutunza vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla hivyo maofisa ambao hawawajibiki watachukuliwa hatua.

Kifungu cha 191 cha Sheria ya mazingira yam waka 2004 kinaeleza kuwa kwa mtu yeyote atakayetiwa hatiani kwa kuivunja ikiwemo kufanya shughuli ndani ya mita 60 katika vyanzo vya maji atapigwa faini isiyopungua Sh50, 000 na isiyozidi Sh50 milioni au kifungo kisichopungua miezi mitatu na kisichozidi miaka saba au vyote kwa pamoja.