Ujenzi wa flyover ya Ubungo wazua jambo

Muktasari:

  • CCECC imesema muundo mpya wa barabara hizo utafanya kazi sawa na ule wa awali, lakini sasa utatekelezwa kwa gharama nafuu na haraka.

 Wakati kampuni ya ujenzi ya CCECC, inayojenga barabara za juu eneo la Ubungo ikisema imebuni muundo mpya wa mradi huo, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), wamesema hakuna mabadiliko yatakayofanyika na mradi huo utatekelezwa kama ulivyopangwa awali.

CCECC imesema muundo mpya wa barabara hizo utafanya kazi sawa na ule wa awali, lakini sasa utatekelezwa kwa gharama nafuu na haraka.

Ujenzi wa barabara hizo za juu katika makutano ya barabara ya Mandela na Morogoro ulizinduliwa Machi 20 mwaka jana na Rais John Magufuli.

Gharama za ujenzi wake ni Sh188.1 bilioni na ilielezwa kuwa utajengwa ndani ya miaka mitatu.

Akizungumza jana wakati wa hafla ya kuwapongeza wafanyakazi wa kampuni hiyo kama sehemu ya maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi, Mei Mosi, Meneja Biashara wa CCECC, Rweyemamu Geragius alisema tayari wamewasilisha muundo huo Tanroads kwa ajili ya mapitio ili kuanza kazi.

Geragius alisema muundo huo mpya umetokana na ubunifu wa mhandisi wa kuongeza thamani ambaye aliona kuwa unaweza kufanyika kwa gharama ndogo zaidi, haraka na ubora uleule.

Pia alisema utatumia eneo dogo la barabara.

“Muundo huu mpya hautawaondoa watu wengine pembezoni mwa barabara, utatoa huduma kwa uwezo uleule na kwa ufanisi zaidi. Tayari tumewasilisha kwa mwenye tenda ambaye ni Tanroads, tunasubiri waupitishe tu,” alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema bado mapendekezo hayo hayajamfikia na kusisitiza kuwa mradi huo utafanyika kama ulivyopangwa awali.

“Mimi ndiye niliyewaajiri (makandarasi), hakuna mabadiliko, mradi utafanyika kama ulivyopangwa na kuandikwa kwenye mkataba,” alisema Mfugale.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atashasta Nditiye alisema hana taarifa za kutosha kuhusu mradi huo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Ufafanuzi wa mkandarasi

Akizungumzia mabadiliko hayo, Geragius alisema iwapo muundo huo utapitishwa, gharama ya ujenzi itapungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hakutaja gharama hizo zitapungua kwa kiasi gani.

“Ukishapitishwa tu baada ya miezi 18 hadi 20 utakuwa umekamilika,” alisema.

Kulingana na mkataba wa ujenzi wa mradi huo, unatarajiwa kuwa na njia tatu; ya chini, ya kati na ya juu.

Njia ya chini ni kwa ajili ya watumiaji wa barabara ya Morogoro – Mjini Kati, ya juu kwa ajili ya magari yatokayo Sam Nujoma kwenda barabara ya Nelson Mandela huku njia ya kati ikiwa ni kwa ajili ya wabadilisha njia.

Katika mabadiliko ya sasa iwapo Tanroads itaridhia, Geragius alisema barabara ya chini itaruhusu muingiliano wa magari na kubadilisha njia.

Alisema barabara ya kati itatumika kwa magari ya Morogoro – Mjini, moja moja bila kusimama na ile ya juu kabisa itatumiwa na magari ya Sam Nujoma na Mandela ambayo yatakwenda moja kwa moja.

Katika hafla hiyo, wafanyakazi wa CCECC walipewa tuzo kwa utendaji wao.

Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Jiang Yigao aliwapongeza waliopewa tuzo na kusema wafanyakazi wa Kitanzania ni muhimu katika kufanikisha mradi huo kwa kuwa bila wao hakuna mafanikio ambayo yangeweza kufikiwa.

“Ushirikiano wetu ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania ya kesho katika kuboresha viwanda, upatikanaji wa nishati na uboreshaji wa miundombinu kama flyover,” alisema Yigao.

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Umoja wa Marafiki wa Tanzania na China, Joseph Kahama aliwaambia wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwa hakuna siri nyingine ya mafanikio zaidi ya kufanya kazi kwa bidii, kujituma na weledi.