Ujenzi wa reli Morogoro mpaka Dodoma kuanza

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco, Masanja Kadogosa

Muktasari:

Reli hiyo itakuwa na urefu wa kilomita 336,wakandarasi 15 walijitokeza baada ya zabuni kutangazwa

Ujenzi wa reli ya umeme kwa kiwango cha standard Gauge wa kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutopora, Dodoma unatarajia kuanza wakati wowote baada ya makubaliano ya saini za ujenzi huo kufanyika.

Makubaliano hayo ya saini yamefanyika leo, Ijumaa Septemba 29 kati ya Kampuni Hodhi ya Rasimali za Reli (Rahco) na Kampuni Yapi Merkezi Inassat Sanayi.s ya nchini Uturuki itakayojenga reli hiyo yenye ukubwa wa kilometa 336.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco, Masanja Kadogosa amesema jumla ya wakandarasi 15 walijitokeza baada ya zabuni kutangazwa lakini Yapi ilionekana kukidhi vigezo vya kiufundi na kifedha na majadiliano hayo yalifanyika kati ya Mei hadi Septemba 25 mwaka huu.

“Jumla ya kilometa ni 336 za njia kuu na kilometa 86 za njia za kupishana treni na maeneo ya kupangia mabehewa yana jumla ya kilometa 422, kwa uzani wa tani 35 kwa eskseli,”amesema Kadogosa.

Amesema baada ya makubaliano hayo mkandarasi huyo atakuwa na jukumu la ujenzi wa miundombinu ya umeme, Morogoro hadi Makutopora na kwenye njia za kupishania na kupangia mabehewa ya treni.

Mbali na hilo atatakiwa kujenga vituo nane vya abiria na vinne vya kupishania treni za mizigo sanjari na ujenzi wa uzio wa kilometa zote za mradi ili kuwapo na usalama wa watu na magari na vivuko vitewekwa kwa matumizi ya waenda kwa miguu, magari pamoja na mifugo.

“Kiwango cha mwendokasi wa treni kitakuwa ni kilometa 160 kwa saa na ujenzi huu utafanyika kwa miezi 36,”amesema Kadogosa.

Kadogosa amesema hiyo ni awamu ya pili ya ujenzi huo baada ya ule wa kwanza wa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kuanza ujenzi na utakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo tani milioni 17 kwa mwaka.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema gharama za ujenzi huo ni zaidi ya Sh trilioni 4 iliyojumlishwa na kodi na kwamba Serikali ingependa kuona mkandarasi akikamilisha mchakato huo chini ya miezi 36.

Amesema kilometa moja ya kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutopora gharama yake ni Sh 3.457 milioni ambapo kiwango hicho kimeongeza tofauti na kila kilometa za kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro  ambacho ni  milioni 3

“Ongezeko hilo limetokana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kipande hiki. Eneo la Kilosa na Mluwe ndiyo yenye matatizo na ndiko tunakoelekea, Pia kuna maeneo korofi matano ambayo yanahitajika kufanyiwa ujenzi.

“Kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kutakuwa na makaravati matano wakati Morogoro hadi Makutopora yatakuwa 143.Upande wa madaraja kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yatakuwa  24 lakini Morogoro hadi Makutopora ni 223 nyie wenywewe mtapima na ,”amesema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ujenzi wa reli haulazimiki kupita katika miamba na milima lakini kutoka Morogoro hadi Makutopora utalazimika kupasua milima katikati ili njia ipatikane.

Amesema gaharama hiyo ni kubwa ukilingnisha na kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni dola za Marekani milioni 3 wakati Morogoro hadi Makutopora ni dola milioni 3.457, hata hivyo gharama hizo bado  ipo chini ukilinganisha na Kenya na nchi zingine zilizojenga reli ya kisasa.

“Kazi yetu kubwa ni kusimamia na kuhakikisha kazi itakayofanywa inaendana na thamani ya fedha,”amesema Profesa Mbarawa.

Makamu Mwenyekiti na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Yapi, Erdem Arioglu  amesema kwa niaba ya bodi ya  hiyo anashukuru kwa hatua hiyo  ya kusaini makubaliano ya ujenzi wa reli ya kisasa ya awamu ya pili na amempongeza Rais John Magufuli kwa jitihada zake.