Ujenzi wa sekondari ya Ihungo, Nyakato kugharimu Sh 60 bilioni

Muktasari:

  • Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu leo mjini Bukoba alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa huo.

Bukoba. Serikali imesema gharama za kujenga upya wa shule za sekondari za Ihungo na Nyakato ni Sh 60 bilioni hadi kukamilika kwa miundombinu yake ambayo itakayoruhusu wanafunzi kupata elimu kama kawaida.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu leo mjini Bukoba alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa huo.

Katika kukamilisha ujenzi wa shule hizo, mkuu wa mkoa amesema kuwa hatua ya kuvunja wa majengo yote imeshaanza ambapo tayari Kampuni ya CHICO ya Wachina inaendelea na uvunjaji wa majengo yote ili kazi ya ujenzi uanze.

“Wataalam wote wa ujenzi kutoka idara mbalimbali za Serikali wanaendelea na uchambuzi yakinifu wa majengo mapya ya shule hizo utakaozingatia viwango vya ujenzi ambapo gharama za awali kwa tathmini iliyotolewa na wataalamu hao ni Sh 30 milioni kwa shule za Ihungo na Nyakato,” alisema Kijuu.

Uamuzi wa kuzijenga shule hizo upya zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi, ulipelekea Serikali kuzifunga na kuwahamisha wanafunzi waliokuwa wanasomea katika shule za Sekondari Ihungo na Nyakato ili waweze kuendelea na masomo wakati shule zao zinajengwa upya.