Ukarabati Ofisi ya Makamu kuchunguzwa

Muktasari:

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa alisema bungeni jana kuwa: “Kamati ilibaini kulikuwa na matumizi yasiyoridhisha ya fedha za umma katika baadhi ya miradi na kuagiza kufanyika uchunguzi maalumu kuhusu matumizi ya fedha na ubora wa miradi.”

Dodoma. Kamati ya Katiba na Sheria, imeagiza mradi wa ukarabati wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam, ufanyiwe uchunguzi ili kujiridhisha na matumizi ya fedha baada ya kubaini kazi imefanyika chini ya viwango.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa alisema bungeni jana kuwa: “Kamati ilibaini kulikuwa na matumizi yasiyoridhisha ya fedha za umma katika baadhi ya miradi na kuagiza kufanyika uchunguzi maalumu kuhusu matumizi ya fedha na ubora wa miradi.”

Mchengerwa aliyekuwa akitoa taarifa ya kazi za kamati hiyo kwa mwaka 2016/17 alisema mradi huo walioutembelea uligharimu zaidi ya Sh2 bilioni.

Alisema wameagiza ufanyike uchunguzi na hatua kali zichukuliwe kwa watendaji waliohusika katika mradi huo iwapo ubadhirifu utabainika.

Mchengerwa alisema ripoti ya uchunguzi wa miradi ya NSSF, ukiwamo wa Dege Eco Village wa Kigamboni, ipo katika hatua za mwisho kukamilishwa na taasisi za uchunguzi. “Kamati ilitoa muda kwa Serikali kukamilisha ripoti hizi na inategemea kupewa taarifa kamili ya uchunguzi.”

Alisema kamati ilikagua mradi wa nyumba za NSSF za Kigamboni- Mtoni Kijichi na imebaini kulikuwa na haja ya Serikali na NSSF kujiridhisha na ukweli au upotoshaji kuhusu tuhuma mbalimbali kwenye miradi hiyo.