Ukawa waja juu ushindi wa CCM

Muktasari:

Lakini, CCM Zanzibar imesema ushindi ilioupata Jimbo la Dimani ni ishara kwamba Watanzania bado wanaendelea kukiamini chama hicho na kukipa dhamana ya kuwaongoza.

Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamelalamikia kuchezewa rafu katika uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani baada ya CCM kuibuka na ushindi, wakiachia kata moja tu.

Lakini, CCM Zanzibar imesema ushindi ilioupata Jimbo la Dimani ni ishara kwamba Watanzania bado wanaendelea kukiamini chama hicho na kukipa dhamana ya kuwaongoza.

Juma Ali Juma aliiwezesha CCM kutetea kiti chake cha ubunge wa Dimani, jimbo pekee lililorudia uchaguzi baada ya kuachwa wazi na Hafidh Ali Tahir aliyefariki dunia Novemba mwaka jana akiwa bungeni mjini Dodoma.

CCM pia imeibuka mshindi katika kata 18 kati ya 19 za Tanzania Bara.