Ukweli kuhusu usalama wa mayai ya kisasa

Muktasari:

Jicho la mjasiriamali ni kufika mbali na hii ndiyo fursa pekee ya kutembea pamoja kwa ubunifu na bidii ya kufuatilia kujua mambo.

Karibu katika uchambuzi na ufugaji wa kuku kwa faida. Tunaendelea kuangazia fursa na njia bora za ufugaji

Jicho la mjasiriamali ni kufika mbali na hii ndiyo fursa pekee ya kutembea pamoja kwa ubunifu na bidii ya kufuatilia kujua mambo.

Ufugaji wa kuku bado ni uti wa mgongo katika dunia ya sasa kwa kutoa mazao ya nyama na mayai kuzilisha jamii zote.

Mtu anapochagua sekta hii amechagua hitaji la watu wengi, hivyo ni vyema kuzingatia kanuni za kitaalamu zitakazomfikisha mbali.

Leo makala itaangazia uzalishaji wa mayai. Utasikia maswali mengi juu ya bidhaa za kuku wa kisasa hususani mayai.

Maswali haya ni kutokana na jamii nyingi kutozoea ufugaji huu wa kisasa. Ukweli ni kwamba, bado kuna jamii zinayapokea mayai ya kuku wa kisasa kwa hisia, zikiamini kuwa uzalishaji wake sio halali.

Aidha, zinaamini kuwa uzalishaji halali wa vifaranga ni mpaka kuku mwenyewe atage na kulalia mayai hadi kuangua vifaranga. Vifaranga wanaototoleshwa kwa njia ya mashine wanaonekana kuwa sio vifaranga sawa sawa kama vifaranga wanaoanguliwa kwa njia ya asili.

Hili ni tatizo la uelewa na ndilo linaloleta mapokeo tofauti na kupunguza imani kwa watumiaji wa mazao haya kutoka kwa kuku wanaozalishwa kisasa.

Mbali na hayo, jamii nyingi zinaamini kuwa kuku hawezi kutaga yai bila jogoo, hivyo kuku wanaotaga mayai bila jogoo hulishwa chakula chenye mbegu za jogoo ili watage.

Huu ni mkanganyiko wa kifikra ambao unahitaji elimu ili watu wafahamu ukweli.

Wito wangu kwa wadau na watumiaji wa mazao ya nyama na mimea ni kwamba tunahitaji kujifunza zaidi ya hapo tulipo. Tukumbuke kuwa dunia iliumbwa kila siku ibadilike kulingana na nyakati.

Huko nyuma wakati mwanadamu anaanza kujitambua, shughuli za kilimo zilianza kwa jembe la mkono kutoka kwa wahunzi katika zama za chuma baada ya zama za mawe na moto kupita.

Ugunduzi uliendelea kila kukicha hadi sasa ukizungumza habari ya kilimo, unaona watu wanatumia mashine kupanda, kupalilia, kuvuna na kusindika mazao.

Ni vizuri kutambua kuwa teknolojia inahitajika kwa ajili ya kuwezesha maisha ya watu kuwa rahisi.

Napenda kuondoa hofu hii juu ya kutumia mayai na nyama za kuku wanaozalishwa kwa njia ya kisasa kuwa ni salama.

Aidha, kuku au vifaranga wanaozalishwa kwa kutumia mashine, ni sawa sawa kabisa na vifaranga tuliowazoea wakizalishwa kwa njia za asili.

Kawaida yai lenye mbegu ya jogoo likiwekwa kwenye mazingira ya joto, ni sawa tu na la mtetea anayepasha mayai yake. Hii ni kwa sababu lazima ikifika siku 21, mayai hayo yataanguliwa.

Kwa hiyo mashine ikitumika kuangua vifaranga, ni jambo la kawaida sawa na mkulima kuacha kutumia jembe la mkono na kutumia mashine kulima au kupanda mazao shambani; mazao hayabadiliki chochote.

Mashine hii ni mwendelezo wa jitihada za binadamu kugundua mbinu mbalimbali za kurahisisha maisha.

Pia kuku wa mayai hahitaji mbegu ya jogoo ili atage, hivyo dhana ya kufikiri kuwa chakula cha kuku wa mayai wanaotaga bila majogoo wanakula chakula chenye mchanganyiko wa mbegu za jogoo ni uongo.

Wafugaji na watumiaji wa mayai wanatakiwa kufuata maelekezo na elimu kutoka kwa wataalamu, badala ya kupata maneno kwa watu wasiojua lolote ambao ni rahisi kuwapotosha.

Mwili wa kuku na ndege wengine majike wakifikia umri wa kutaga huzalisha mayai bila kujali uwepo wa jogoo ili watage.

Kuwepo au kutokuwepo kwa mbegu za jogoo kwenye yai, hakuhusiani na yai kutengenezwa au kutagwa.

Pia watu hudhani kuwa yai lisilo na mbegu ya jogoo sio yai bora kwa mlaji kwa sababu limekosa mbegu ya jogoo. Sio kweli.

Mbegu ya jogoo haina mchango wowote kwenye yai la kula. Mbegu ya jogoo inahitajika kwenye yai pale tu mfugaji anapotaka kupata kifaranga.

Kwa utani watu husema mtu anayekula mayai ya kisasa au mayai ya kuku wasio na jogoo eti wanakula mayai yasiyo na baba!

Hii ni kejeli mbaya kwa watumiaji na ipuuzwe. Pengine kejeli hii inaweza kuwa ni utani tu, lakini mtu asiyeelewa anaweza kuamini kuwa mayai hayo sio bora kwa walaji.

Ifahamike kuwa jogoo sio baba wa yai bali ni baba wa kifaranga kwa kuweka mbegu yake kwenye yai lililokamilika. Kuku akitaga yai bila jogoo yai hilo halitatoa kifaranga lakini ni yai bora kwa chakula.

Ukisikia habari ya yai tupu ndiyo hii. Hili ni yai lisilokuwa na mbegu ya jogoo; halifai kuatamishia lakini linafaa kwa kula.

Kupitia makala haya pia ni vema watumiaji wa mayai waelewe vizuri kitu wanachokitumia kuwa ni salama. Dhana ya chakula au teknolojia inayotumika kuzalisha vifaranga pamoja na chakula wanachopewa, huo ni ubunifu wa kijasiriamali uliofanyika kurahisisha maisha kwa kutumia teknolojia.

Tunapenda watu wazidi kubuni na kuleta njia mpya za ujasiriamali kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya taifa letu.