Ulega ataka Watanzania wasifuge kuku kwa mazoea

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Muktasari:

Watanzania waondokane na tabia ya kufuga kuku kwa mazoea na badala yake wafuge kiniashara ili kujikwamua kiuchumi na kuikuza sekta hiyo

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema ni wakati muafaka kwa Watanzania kuondokana na tabia ya kufuga kuku kwa mazoea na badala yake wafuge kibiashara ili kujikwamua kiuchumi na kuikuza sekta hiyo.

Ulega ameeleza hayo leo Ijumaa Septemba 21, 2018, wakati akifungua mafunzo ya siku  moja ya wafugaji wa kuku wa kisasa wa mkoa wa Dar es Salaam.

Naibu waziri huyo amesema ni watu wachache wanaofuga kuku kibiashara, lakini wengi wanafuga kama sehemu ya maisha yao, hali inayosababisha kutofikia malengo yao hasa ya kutambua fursa zilizopo za sekta hiyo.

“Hapa Dar es Salaam nataka mfuge kibiashara, hatutaki mfuge kuku kimazoea. Tunataka watu wajue ufugaji kuku ni biashara kama zingine na ni fursa ambayo ikitumika vyema inabadilisha maisha yao kwa kiwango kikubwa,” amesema Ulega.

Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Mkuranga amesema ufugaji wa kuku hasa wa kisasa ni sehemu mojawapo itakayowakomboa vijana na wanawake kuondokana na tatizo la ajira ambalo limekuwa kilio cha wengi.

Amesema nyama ya kuku inapendwa kila mahali na kwenye miradi mikubwa ya maendeleo wanaitumia kama kitoweo chao hivyo,  ni vyema wafugaji wakaione fursa hiyo kwa kuzalisha kwa wingi ili kuchangamkia fursa hiyo.

“Tunataka watu wazalishe kuku wa kutosha ili nyama yake ishuke bei. Maana sasa hivi baadhi ya watu kula kwao nyama hii hadi kuwe na shughuli fulani au sherehe jambo ambalo halileti picha nzuri hasa kwa karne hii ya uchumi wa viwanda unaohimizwa na Rais John Magufuli,” amesema.

Ulega ametumia nafasi kuwaeleza washiriki wa mafunzo hayo, wajisikie huru kuuliza maswali yoyote kwa wahusika kuhusu sekta ya kuku, changamoto zake na namna ya kukabuliana nazo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo ya Ugavi wa wizara hiyo. Dk Angelo Mwilawa amesema mafunzo hayo yameshirikisha wataalamu kutoka wilaya tano za  Kigamboni, Ilala, Temeke, Kinondoni na Ubungo.

Amesema lengo la mafunzo hayo kuwajengea uwezo wafugaji hao wa namna ya kufuga kuku kibiashara badala ya mazoea sanjari na kuwafundisha mbinu za kuyafikia masoko mbalimbali na kuwaunganisha katika mitandao itakayorahisisha shughuli zao.

Mmoja wafugaji akizungumza kwa niaba ya wenzake, Eva Nyella mafunzo yatawasaidia kiasi kikubwa kuimarisha sekta hiyo ili ipige hatua za maendeleo.