Ummy Mwalimu alia na gharama za matibabu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu 

Muktasari:

Azitaka hospitali kuangalia namna ya kupunguza gharama za matibabu


Dodoma. Waziri wa Afy, Ummy Mwalimu amezitaka hospitali nchini kutafuta njia bora za kupunguza gharama zake za matibabu.

Akizungumza jana Juni 22, 2018 katika uzinduzi wa bodi ya wadhamini wa Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini hapa, Ummy amesema katika uongozi wake kwenye wizara hiyo, gharama za matibabu ni jambo linalompa wakati mgumu.

Amesema amekuwa akipokea simu kutoka kwa watu mbalimbali wakilia na gharama kubwa za matibabu jambo ambalo limekuwa likimuumiza kwa muda mrefu.

Alimtaka mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Alfonce Chandika kuanza kuonyesha katika suala hilo katika utendaji wake ili wengine wajifunze kupitia kwake na kuwataka wananchi kuitumia hospitali hiyo kutibiwa magonjwa makubwa.

Dk Chandika amesema hospitali hiyo ilianzishwa kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu ya figo, moyo, macho, upasuaji wa matundu madogo na kutumika kama hospitali ya mafunzo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Amesema huduma nyingine zilizoanza kutolewa ni upasuaji wa tezi dume, usafishaji damu, huduma ya upandikizaji figo pamoja na uchunguzi na matibabu ya moyo kwa kutumia maabara maalumu.

Amebainisha kuwa licha ya mafanikio hayo, bado hospitali hiyo tegemeo mkoani hapa inakabiliwa na changamoto za upungufu wa watumishi, makazi na kwamba waliopo kwa sasa hawafikii asilimia 50 ya mahitaji.