Ummy Mwalimu azitaka halmashauri kutenga fedha za wanawake na vijana

Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia,wazee na watoto, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi

Chamwino. Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vyawanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.

 Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia,wazee na watoto, Ummy Mwalimu kwenye maadhimisho ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Kijiji chaManchali B, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Maelezo ya Ummy yalisomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk John Jungu.

Mwalimu amesema kuwa Serikali imetoa fursa nyingi kwa wanawake  katika kuboresha maisha yao wanaoishi vijijini kwa kuwa inatambua kuwa ndiyo wazalishaji wakubwa wa chakula si nchini tu bali duniani kote.

“Serikali ina mifuko mingi ya uwezeshaji ambayo inafanya kazi hapa nchini lakini niutaje mfuko mmoja tu wa maendeleo ya wanawake ambao uko chini ya Wizara ya afya, huu ni maalum kwa ajili ya kuwawezesha wanawake ambapo mpaka sasa zaidi ya Sh16.3 bilioni zimeshatolewa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake nchini,” amesema Mwalimu.

“Na fedha hizi ni zile asilimia nne ambazo zinatengwa na Halmashauri kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha vikundi vya wanawake, vijana na watu na wenye ulemavu.”

 Amesema Serikali pia inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini ili ziweze kupitika kwa kipindi chote cha mwaka, kuimarisha upatikanaji wa maji vijijini kuboresha huduma za afya vijijini hasa katika kujenga zahanati na hospitali za Wilaya nchi nzima.

Lucy Letona mkazi wa Kijiji cha Manchali B amesema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakisikia serikali inatoa fedha kwenye vikundi vya wanawake lakini fedha hizo  haziwafikii kwa kuwa hata wao wako kwenye vikundi vya wakulima na bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa soko la mazao yao.

Magreth Mazengo ameiomba serikali kuboresha huduma za afya

vijijini kwa kuwa wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya hali inayosababisha watoto wengi wa kike kutorokea mijini baada ya kumaliza masomo yao ili wakapate huduma bora za afya.

Maadhimisho hayo ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini imefanyika kwa mara ya kwanza kitaifa nchini ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni  kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe miundombinu na huduma za jamii kwa wanawake na wasichana waishio vijijini.