Upelelezi kesi ya kina Kitilya haujakamilika

Muktasari:

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha, wanaendelea kusota rumande kwa takribani miaka miwili sasa kutokana upelelezi kutokamilika

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia  uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na waliokuwa maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Mori Sinare na Sioi Solomon wanasota rumande kutokana na upande wa mashtaka kuendelea kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Upendo Temu amesema leo Septemba 14, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa lakini upelelezi bado, kuomba ipangiwe tarehe nyingine.

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha, wanaendelea kusota rumande kwa takribani miaka miwili sasa kutokana upelelezi kutokamilika.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 28, 2018.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani 550 milioni  kwa  serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.

Wanadaiwa kuwa  Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani 6 milioni, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo  na zililipwa kupitia  Kampuni ya Egma T Ltd.

Washtakiwa  hao wanadaiwa  kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni katika akaunti tofauti tofauti  za benki.

Kati ya  Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa  kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.