Upinzani Kigoma wadaiwa kuchochea maendeleo

Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Halima Mdee

Muktasari:

Katibu wa Bawacha Mkoa wa Kigoma, Lydia Daudi aliliambia gazeti hili mjini hapa kuwa, baada ya upinzani kuanza kushika hatamu mkoani humo, ndipo Serikali ilianza kujenga barabara kwa kiwango cha lami.

Kigoma. Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Mkoa wa Kigoma limesema maendeleo mkoani humo yameonekana baada ya upinzani kushinda majimbo mengi mwaka 2010.

Katibu wa Bawacha Mkoa wa Kigoma, Lydia Daudi aliliambia gazeti hili mjini hapa kuwa, baada ya upinzani kuanza kushika hatamu mkoani humo, ndipo Serikali ilianza kujenga barabara kwa kiwango cha lami.

“Kigoma iliachwa nyuma katika nyanja za miundombinu, hali iliyoufanya mkoa huo kuwa kama kisiwa kutokana na kukosa barabara za lami za kuunganisha na mikoa mingine jirani ya Tabora, Katavi na Kagera, hivyo kufanya usafiri kuwa wa shida hasa kipindi cha mvua,” alisema.

Aliutaja ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Kigoma chenye urefu wa mita 1,720 kwa kiwango cha lami na Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi.

Pia, alisema kumekuwapo na ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 220 na nyingine zikiwa kwenye mchakato wa ujenzi na kwamba hayo ni matokeo ya wananchi kuchagua wabunge na madiwani kutoka vyama vya upinzani.