El Hadji Diouf afuata nyayo za George Weah

Muktasari:

Mchezaji huyo wa zamani mwenye makeke alitangaza mwaka jana kuwa anataka kuwa mbunge lakini baada ya Weah kuwa rais, anaweka vitu vyema zaidi ili aweze kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi.

 

 

 


Dakar, Senegal. Mwanasoka nyota wa zamani wa kimataifa wa Senegal na Liverpool, El Hadji Diouf anataka kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2019 akifuata nyayo za gwiji George Weah ambaye amechaguliwa kuwa rais wa Liberia.

Diouf, mwenye umri wa miaka 37 na ambaye aliichezea Leeds United ya Uingereza kwa misimu miwili tangu aliposajiliwa na kocha mkuu Neil Warnock mwaka 2012 amesema amepata hamasa kutokana na mafanikio ya kisiasa ya Weah.

Mchezaji huyo wa zamani mwenye makeke alitangaza mwaka jana kuwa anataka kuwa mbunge lakini baada ya Weah kuwa rais, anaweka vitu vyema zaidi ili aweze kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi.

"Ninajiangalia mwenyewe na familia yangu. Kwa miaka mingi nimekuwa nikifikiria juu ya mpira wa miguu lakini kwa sasa nina kazi mpya na ni kazi ya kisiasa," alisema Diouf.

“Nimeamua kufanya siasa kwa sababu nina watu wanasubiri kuona nikibadili mambo katika nchi yangu na niko tayari kufanya hivyo kwa sababu nataka kuwa askari wa vijana."

Mwaka jana Diouf alibainisha kuwa anaachana na mipango ya kuwa kocha kwa sababu kwake kazi ya siasa ina mvuto zaidi.

Alisema: "Mustakabali wangu uko wazi. Katika miaka miwili ijayo nitajiunga na siasa, kwa sababu najua kuanzia hapo nitaweza kubadilisha mengi katika soka. Ninatamani sana siasa, na nina watu huko Senegal ambao wananiongoza. "Hayo ni maisha yangu ya baadaye, kwa sababu watu wengi nchini Senegal wanaweza kunisikiliza.”

Diouf mwenye uraia wa Ufaransa na Senegal, ameorodheshwa kuwa mtu wa tatu maarufu zaidi nchini Senegal, hali ambayo kwa sasa inamuwasha kujitosa kwenye siasa. Kadhalika ameorodheshwa kuwa wa 7846 katika usakataji kabumbu.

Anafahamika vyema kwa hasira za haraka na aliwahi kutemea watu mate mara kwa mara uwanjani. Mwaka wa 2003, alishtakiwa Uingereza kwa kumtemea mate shabiki wa klabu ya Celtic na akatozwa faini sawa na kitita chake cha pato la jumla kwa wiki mbili mfululizo.

Mwaka wa 2004, alishtakiwa tena kwa kumtemea mate kijana wa miaka 11 na shabiki wa timu ya Middlesbrough na pia akapigwa marufuku ya mechi tatu mfululizo kwa kumtemea mate beki wa Portsmouth, Arjan de Zeeuw.