Usajili vyeti vya kuzaliwa sasa kwa njia ya simu za mkononi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akikabidhi cheti jana cha kuzaliwa kwa mmoja wa mzazi wa mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano aliyesajiliwa katika mpango maalumu wa utoaji vyeti vya kuzaliwa  bure katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

  • Ongezeko la mikoa hiyo unafanya jumla ya halmashauri zinazonufaika na mpango huo nchini kufika tisa. Katika mikoa saba ambako mfumo huo unatumika, zaidi ya watoto milioni 1.6 wamenufaika.

Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Tigo imezindua usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Ongezeko la mikoa hiyo unafanya jumla ya halmashauri zinazonufaika na mpango huo nchini kufika tisa. Katika mikoa saba ambako mfumo huo unatumika, zaidi ya watoto milioni 1.6 wamenufaika.

Akizindua mpango huo, Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe alisema cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila mtoto na ni muhimu katika kupanga maendeleo kwa kuwa takwimu sahihi zinahitajika kuifanikisha.

“Takwimu zinaiwezesha Serikali kujua mahitaji yaliyopo. Mpango huu utatuondoa katika ukisiaji kwa kuwa unawasiliana na kanzidata ya (Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo) Rita,” alisema Dk Mwakyembe.

Kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huo mwaka 2012, takwimu zinaonyesha watoto waliokuwa wanapata vyeti vya kuzaliwa walikuwa asilimia kumi na moja, lakini mikoa inayonufaika mpaka sasa imeongeza hadi kufikia zaidi ya asilimia 90.

“Vyeti vinavyotolewa vimejazwa kwa mkono na haviwezi kughushiwa. Taasisi za umma na binafsi zivitambue kwa kuwa ni halali,” alisema Dk Mwakyembe.

Kufanikisha mpango huo, Tigo imetoa simu 1,000 za kisasa (smartphones) zenye thamani ya Sh95 milioni. Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo ya mawasiliano, Simon Karikari alisema teknolojia ya simu za mkononi ni muhimu katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

“Serikali inaweza kufuatilia usajili wa vizazi kwa urahisi zaidi kuanzia vijijini na kujua muda, mahali, umri hata jinsia ya kila mtoto anayesajiliwa kutoka popote nchini, hivyo kurahisisha matumizi ya taarifa hizi. Haya yote yasingewezekana kama si kwa ushirikiano,” alisema Karikari.

Karikari alisema umuhimu wa vyeti hivyo ni pamoja na kuwezesha kupata nyaraka nyingine za umma kama vile kitambulisho cha taifa, mpigakura, hati za kusafiria au leseni ya udereva na hata leseni za kampuni za biashara.

“Leo hii huwezi kusajili laini ya simu bila kuwa na vitambulisho nilivyovitaja. Tigo itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa wanasajiliwa ifikapo mwaka 2021,” alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya Rita, Profesa Hamis Dihenga alisema utafika wakati itakuwa ni lazima kila mwananchi kuwa na cheti cha kuzaliwa.

“Utafikia wakati hata kuanza shule cheti hiki kitahitajika ili watoto watambulike,” alisema Profesa Dihenga.

Aidha, alisema takwimu za usajili wa watoto katika mikoa ya Lindi na Mtwara zipo chini, akibainisha kwamba ni asilimia kumi na moja ya watoto wa Lindi ambao wamesajiliwa na asilimia 9.4 Mtwara.

Tayari mpango huo unaofadhiliwa na serikali ya Canada na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) unatekelezwa Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Songwe, Iringa, Geita na Njombe.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aliitaka Serikali kuendelea kutenga bajeti ili mpango huo uwe endelevu.

“Tutautekeleza mpango huu kwa ufanisi na kuwa mfano kwa mikoa mingine,” alisema.