Ushindani ni mkubwa matokeo darasa la saba

Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde akionyesha karatasi ya mtihani wa darasa la saba iliyosahihishwa kwa mfumo wa kompyuta jijini Dar es Salaam. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Pamoja na kuwapo udanganyifu kwa baadhi ya shule, matokeo yanaonyesha kuongezeka ufaulu kutoka asilimia 4.96 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka uliopita huku shule zilizotamba matokeo yaliyopita zikishindwa kufurukuta.



 

Dar er Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba 5 na 6 mwaka 2018 ambayo yameshuhudia udanganyifu ukifanywa kwa baadhi ya shule na wengine wakifutiwa matokeo.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana jijini Dar es Salaam na katibu mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, yameonyesha ushindani mkubwa na mabadiliko ya shule zilizotinga kumi bora kitaifa, safari hii nyingi zikitoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Pia, matokeo hayo yameshuhudia nafasi ya mwanafunzi bora kitaifa ikichukuliwa na Ndemezo Lubonankebe wa Shule ya Kadama mkoani Geita wakati mwaka jana, aliyeshika nafasi hiyo alikuwa Hadija Aziz Ali kutoka Sir John ya jijini Tanga.

Matokeo hayo yanaonyesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 4.96 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana yaliyokuwa asilimia 2.40. Dk Msonde alisema katika ngazi ya ufaulu kwa mikoa, Dar es Salaam imeongoza kwa asilimia 92.26 ikifuatiwa na Geita yenye asilimia 88.53.

Kwa upande wa Halmashauri, Arusha Mjini imeongoza kwa ufaulu wa asilimia 97.43 ikifuatiwa na Moshi Mji yenye ufaulu wa asilimia 96.21.

Dk Msonde alisema ufaulu umefikia asilimia 77.12 kutoka asilimia 72.76 ya mwaka jana.

Alisema awali jumla ya watahiniwa 957, 904 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambapo kati ya hao 733,103 wamefaulu mtihani huo wakiwemo wasichana 382,830 (asilimia 77.12) na wavulana 350,273 (sawa na asilimia 78.38).

“Takwimu zinaonyesha ufaulu katika masomo ya Kiingereza, Maarifa ya Jamii, Hisabati na Sayansi umepanda kwa asilimia kati ya 4.03 na 11.92 ikilinganishwa na mwaka 2017,” alisema Dk Msonde.

Hata hivyo, alisema katika somo la Kiswahili ufaulu umeshuka kwa asilimia 1.44 licha ya somo hilo kufaulisha kwa asilimia 85.42 huku wakifanya vibaya katika somo la Kiingereza lenye ufaulu wa asilimia 49.63.

Kanda ya Ziwa yang’ara

Katika matokeo hayo, shule zilizopo mikoa ya Kanda ya Ziwa zimefanya vizuri katika maeneo mbalimbali ikiwamo kutoa shule nane kati ya kumi bora kitaifa.

Wakati shule ya Raskazone ya mkoani Tanga ikishika namba moja kwenye shule kumi bora kitaifa, Mkoa wa Kagera umetoa shule nne (J.Kibira, St.Achileus Kiwanuka, St. Severine na Rweikiza), Shinyanga mbili (Kwema Modern na Rocken Hill).

Mwanza imeingiza shule ya Nyamuge na mkoa wa Mara una shule ya Twibhoki. Dar es Salaam ina shule moja ya St Anne Marie wakati mwaka jana ilikuwa na shule mbili.

Shule saba za 2017 chali

Katika shule zilizotinga kumi bora mwaka jana, ni shule tatu tu ndizo zimefanikiwa kubaki kundi hilo mwaka huu ambazo ni Rweikiza, St Severine na St Anne Marie.

Shule saba za mwaka jana zilizokuwa kwenye kumi bora, lakini zimetupwa nje ya kundi hilo mwaka huu ni Alliance (Mwanza), Palikas (Shinyanga), Mwanga (Kagera), Hazina (Dar es Salaam), Martin Luther (Dodoma), St Peter (Kagera) na St John (Tanga).

Shule kumi zilizofanya vibaya mwaka jana, zote zimeondoka katika kundi hilo na kuziacha shule nyingine zikikaa hapo.

Zilizoshika mkia ni Mangika (Tanga), Mwazizi (Tabora), Isebenda (Simiyu), Malagano (Tabora), Magana (Mara), Kodoo (Morogoro), Mtindili (Tanga), Lumalu (Ruvuma), Chidete (Dodoma) na Mavului ya Tanga.

Mwaka jana zilizoshika mkia zilikuwa Nyahaa (Singida), Bosha (Tanga), Ntalasha (Tabora), Kishangazi (Tanga), Mnamba (Singida), Ikolo (Singida), Kamwala (Songwe), Kibutuka (Lindi), Mkulumuzi (Tanga) na Kitwai A ya Manyara.

Udanganyifu ulivyokuwa

Akitangaza matokeo hayo jana, Dk Msonde alianza kwa kutaja dosari mbalimbali zilizojitokeza katika mtihani huo ikiwamo wizi wa mitihani pamoja na udanganyifu ambao umesababisha wanafunzi 357 kufutiwa matokeo.

Oktoba 2, baraza hilo lilitangaza kufuta matokeo ya shule zote za halmashauri za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma, Shule za msingi Hazina na New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za Dar es Salaam pamoja na Alliance na New Alliance za Mwanza kwa tuhuma za kuvujisha mitihani.

Jana, Dk Msonde alisema uchunguzi uliofanyika na baraza hilo umebaini wizi wa mtihani ulifanyika katika kituo teule cha Nyanduga kilichopo Halmashauri ya Rorya mkoani Mara.

“Baraza limejiridhisha ushiriki wa shule zote hizi wakiwamo wamiliki wa shule pamoja na walimu wao kuhakikisha wanaupata mtihani ule katika kituo teule cha Shule ya Msingi Nyanduga kilichopo Halmashauri ya Rorya mkoani Mara,” alisema.

“Mtihani ule kutoka kituo cha Nyanduga ulirushwa usiku uleule mapema kabla ya siku ya mtihani na ukaenda kwenye shule ya Fountain of Joy na Aniny Nndumi na walimu hawa walipopata ule mtihani wakaendelea kusambaza kwenye shule nyingine,” alisema Dk Msonde.

Alisema shule hizo zilishirikiana na baadhi ya viongozi wakiwamo maofisa elimu, wasimamizi pamoja na walinzi kwenye kituo hicho katika kuhakikisha wanaupata mtihani kwa ajili ya kuwapa wanafunzi kwenye shule zao.

Aliwataja viongozi hao akiwamo ofisa elimu msingi, Zacharia Weibina na Thobias Ojijo ambaye ni ofisa elimu vifaa na takwimu ambaye wakati wa tukio alikuwa kaimu ofisa elimu wa halmashauri hiyo.

Pia, ofisa elimu kata Omary Kilo ambaye alikuwa mkuu wa msafara wa kusafirisha mitihani kwenda vituo vingine jirani.

Wengine ni mkuu wa Shule ya Nyanduga, Marwa Mtatiro pamoja na msimamizi mkuu wa kituo, Emma Macha na mlinzi wa kituo mwenye namba G6098DC aliyetajwa kwa jina la Gisbert.

Dk Msonde alisema kituo cha Nyanduga kilikuwa kinalisha vituo saba vya jirani ndani ya halmashauri hiyo na kituo cha mbali zaidi kilikuwa ni kilomita 16 kutoka kituo kikuu cha Nyanduga.

“Kwa makusudi mazima huyu mkuu wa msafara alijifanya yeye kwamba afungue mitihani na aisambaze kwenye vituo saa saba usiku, lakini unaweza ukajiuliza unasafiri saa saba usiku na una gari kwenda kilomita 16?” alisema.

Alisema hiyo ilikuwa kama ‘danganya toto’ kwakuwa walikuwa tayari wamefanikisha kufungua mitihani hiyo kabla ya kuanza kazi ya usambazaji kwenda vituo vingine.

“Kwa hiyo ile saa saba usiku ilikuwa danganya toto lakini kazi ilikuwa imefanyika mapema,” alisema.

Kufuatia sakata hilo, Dk Msonde alisema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika kulingana na mamlaka zinazowasimamia.

Pamoja na hayo, Dk Msonde alisema wakati mitihani inafanyika kulikuwapo na udanganyifu uliofanywa na wanafunzi wakiwezeshwa na wasimamizi wa mitihani pamoja na walimu ikiwamo kuwapa majibu.

Alisema kufuatia hatua hiyo, jumla ya wanafunzi 357 wamefutiwa matokeo yao hivyo kutotambuliwa na baraza hilo kama wamehitimu elimu ya msingi.

Alisema baadhi ya dosari zimejitokeza hasa baada ya usahihishaji wa mitihani na baadhi ya shule zilikuwa na majibu yanayofanana huku wengine wakikutwa na majibu yaliyoandikwa kwenye rula ndani ya vyumba vya mitihani.

Alitaja baadhi ya vituo vilivyokumbwa na kadhia hiyo ikiwamo Shule ya Msingi Liwale mkoani Lindi ambapo mwalimu mkuu, Rusiasi Matembo anadaiwa kula njama na wasimamizi ili kutoa mitihani nje na kuikokotoa ili kuwapa majibu wanafunzi.

“Wakati watahini wanasahihisha mitihani hii walibaini kuwa katika shule ya msingi Mwekako ya mkoani Geita wanafunzi waliandika kwenye karatasi tofauti na ile waliyopewa na baraza,” alisema Dk Msonde.

Shule ya msingi Bariadi Alliance ya mkoani Simiyu pamoja na Msufini ya mkoani Geita zilibainika kuwa na watahiniwa kuandika majibu yanayofafa karibu mtihani mzima wa Hisabati na Kingereza.

Wanafunzi kumi bora

Licha ya Kanda ya Ziwa kutoa shule nane kati ya kumi bora kitaifa, katika kundi la wanafunzi kumi bora, sita kati ya kumi wanatoka shule za mikoa ya kanda hiyo.

Dk Msonde aliwataja wanafunzi hao bora kuwa ni; Ndemezo Lubonankebe (Kadama-Geita), Innocent Seleli (Carmel- Morogoro), Given Malyango (Tumain Junior- Arusha), Diomedes Mbogo (St. Archileus Kiwanuka- Kagera) na Sweetbert John (Mingas- Shinyanga).

Wengine ni Najma Manji (Nyamuge-Mwanza), Beatrice Jeremiah (Mapinduzi B- Mara), Mohamed Mohamed (Raskazone-Tanga), Luqman Ally (Raskazone-Tanga) na Francisco Maiga (kadama-Geita).