Ushuru wa korosho bado watikisa mjadala wa bajeti

Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kutoingia katika historia ya kuliua zao hilo.

Dodoma. Hoja ya Serikali kurudishwa asilimia 65 ya fedha zinazotokana na ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi imeendelea kutikisa mjadala wa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kutoingia katika historia ya kuliua zao hilo.

Akichangia mjadala wa Bajeti jana, Chikota alisema kwa miaka mitatu uwekezaji uliofanyika uliinua uzalishaji wa korosho mara mbili lakini kinachomsikitisha sasa ni mambo yanayolenga kulidhoofisha zao hilo.

Alisema kwa pamoja, wabunge wa mikoa ya Kusini walikwenda kwa Dk Mpango kuzungumzia upatikanaji wa fedha za pembejeo na aliwajibu kuwa kuna tatizo katika sheria ya korosho kwa sababu ilipaswa kuanza kutumika baada ya kutengenezwa kanuni.

“Matokeo yake ni kuwa ile sheria ya korosho ambayo inasema kuwa asilimia 35 ya Export Levy (ushuru wa mauzo ya nje) utakwenda mfuko mkuu wa Serikali inakwenda kufutwa na nimechungulia katika Finance Bill (muswada wa sheria ya fedha) inafutwa ili pesa zote ziingie katika mfuko mkuu,” alisema.

“Hapa mnaua korosho. Hapa mnafanya siasa ya mikoa ya Lindi na Mtwara iwe ngumu. Ndugu zangu waheshimiwa wabunge tuungane, kwa taarifa ya kituo cha Utafiti cha Naliendele sasa hivi wamejikita katika mikoa 17. Wale wenzangu wa Tabora wa Chunya fedha hii ikiondoka hamtawaona wataalamu wa Naliendele wanakuja kwenu,” alisema.

Aliwataka wabunge kutoka mikoa 17 inayolima zao hilo kuungana ili wapigakura wao waweze kupata matunda yanayotokana na wataalamu wa kituo hicho cha utafiti.

Alisema madhara ya kukosekana kwa fedha hizo ni upungufu wa miche ya korosho, kushindwa kuendeleza maeneo mapya na kupotea kwa ajira za watumishi.

Chikota alisema kituo cha Naliendele kina waajiriwa 77, kati yao madereva wawili ndio watumishi wa kudumu huku wengine wakitegemea kulipwa na fedha zinatokana na ushuru wa mauzo ya nje ya korosho.

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Nachuma Maftaha aliitaka Serikali kutoa fedha za ushuru huo, Sh210 bilioni kwa wakulima.

“Wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi ambao ndio wakulima wa korosho, mwaka huu wamekosa salfa wanataka fedha ziletwe hata kama ni kwa mwaka ujao wa fedha la sivyo wataandamana,” alisema.

Alimuomba Rais John Magufuli kufika Mtwara kupokea maandamano makubwa ya wananchi wanaolalamikia kuhusu kupokwa kwa haki yao.

Mbunge wa Nachingwea (CCM), Hassan Masala alisema mwaka 2015 walipendekeza namna ya kuboresha mazao ikiwamo korosho ili kuongeza tija kwa wakulima na Taifa kwa jumla na hasa kwa kuondoa tozo.

“Nimepata shaka juu ya mapendekezo ambayo Waziri Mpango umeyaleta. Jambo hili kwetu sisi wakulima hamtakuwa mmetusaidia, hebu fikiria kuliondoa kwani unataka kutugombanisha na wananchi,” alisema Masala.

“Haya mapendekezo hayana tija na hayatatusaidia kabisa, Waziri Mpango hujasema zile fedha za nyuma wakulima wanazipataje unaleta mapendekezo. Tutaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali lakini katika hili la kuua zao la korosho hatutakubali,” alisema.

Juzi, mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu Bwege alisema fedha zisipotolewa hadi Juni 30 wataandamana akimwomba Spika Job Ndugai kupokea maandamano yao.

Kauli za wakulima

Kilio hicho hakikuishia bungeni, mkulima Elisha Millanzi, mkazi wa Nanyumbu mkoani Mtwara alisema kutotolewa fedha kutasababisha bodi kushindwa kujiendesha na kutoa huduma ya kwa wakulima.

“Nashauri basi igawanywe asilimia 50 kwa 50, leo hii kuna kufuatilia dawa na ukizingatia hutapuliza aina moja, kila mwaka unakutana na aina tofauti za mikorosho nayo inaleta magonjwa sidhani kama Serikali inaweza kutuletea watu wa kufanya tafiti za hiyo mikorosho kama wanavyofanya watu wa bodi kwa kushirikiana na watafiti wengine,” alisema.

Mkulima mwingine, John Joseph kutoka Tandahimba alisema kama fedha yote itakwenda serikalini, bodi italazimika kupata fedha kutoka Wizara ya Kilimo ambayo nayo bajeti yake haitoshelezi mahitaji.

Diwani wa Chilangala Wilaya ya Newala, Jamali Nandonde alisema kama Serikali imeamua kubadili sheria, ni vyema wakapatiwa fedha za msimu wa mwaka 2016/17 na 2017/18.

“Serikali haki yake ilikuwapo asilimia 35 na wakulima ilikuwapo asilimia 65 sasa inataka ichukue na ya wananchi maana yake ni nini? Hili ni tatizo,” alisema.

Nyongeza na Haika Kimaro