Ushuru wa mnara wawagonganisha viongozi

Muktasari:

  • Hata hivyo, Kampuni ya Simu ya Halotel inayomiliki mnara huo imepinga madai hayo ya viongozi wa vijiji hivyo, ikisema inamtambua mtu mmoja mwenye ardhi na waliyeingia naye mkataba wa malipo.
  • Ofisi ya Ardhi ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, imeingilia kati na kupitia mipaka upya hivyo kubaini mnara upo Berege siyo Gulwe.

Mpwapwa. Mnara wa simu uliojengwa mpakani mwa vijiji vya Berege na Gulwe wilayani hapa, umeibua mgogoro ikidaiwa chanzo ni ushuru kutolipwa kwa walengwa.

Hata hivyo, Kampuni ya Simu ya Halotel inayomiliki mnara huo imepinga madai hayo ya viongozi wa vijiji hivyo, ikisema inamtambua mtu mmoja mwenye ardhi na waliyeingia naye mkataba wa malipo.

Ofisi ya Ardhi ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, imeingilia kati na kupitia mipaka upya hivyo kubaini mnara upo Berege siyo Gulwe.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Berege, Mathias Elia na kiongozi wa Baraza la mila, Ashery Kamwaya juzi walifika ofisi za Halotel mjini Dodoma wakiwa na vielelezo lakini waligonga mwamba.

Elia alisema uongozi wa kampuni hiyo umekataa kuwalipa au kuingia nao mkataba kwa sababu hawawatambui. “Tumeleta vielelezo na ofisi ya mkuu wa wilaya ilishatoa ushahidi kuwa eneo lile ni la Kijiji cha Berege, hivyo hawa watu walipaswa kuingia mkataba na kijiji lakini wamegoma,” alisema Elia.

Mkurugenzi wa Halotel Dodoma, Rista Manyara alisema hawezi kuwalipa au kuingia mkataba na Serikali ya kijiji chochote kati ya hivyo, badala yake ataendelea kumtambua waliyeingia naye mkataba tangu awali. “Suala kuwa mnara umejengwa wapi sisi halituhusu kwa kuwa mtu anaweza kuishi mjini na akawa na shamba kijijini, ndiyo maana nitaendelea kumlipa yule wa awali,” alisema Manyara.

Mtu anayedaiwa kuwa mmiliki wa eneo hilo, Japhet Sabugo aliandika barua na kupitishwa na Mtendaji wa Kijiji cha Gulwe, Cyprian Challo kueleza kujitoa katika eneo hilo ili Berege waendelee kulipwa, lakini kampuni hiyo imeshikilia msimamo wa kutoutambua uongozi huo.