Uzalendo, utiifu misingi mikuu ya utaifa

Rais John Magufuli akisikiliza maelezo ya Mwenyekti wa kamati ya kuchunguza mchanga wa madini, Profesa Abdulkarim Mruma Ikulu hivi karibuni. Anayetazama ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Taifa lenye utii, kujenga uzalendo ni kazi rahisi. Itoshe kusema Watanzania wana nia njema na nchi yao lakini kwa kukosa ufahamu wa mambo mengi wanajitokeza wajanja wachache wenye nia ovu wanaofanya upotoshaji.

Kanuni namba moja ni utii kwanza, maswali baada ya utii. Kanuni namba mbili ikiwa una mashaka na amri hii, rejea kanuni namba moja.

Taifa lenye utii, kujenga uzalendo ni kazi rahisi. Itoshe kusema Watanzania wana nia njema na nchi yao lakini kwa kukosa ufahamu wa mambo mengi wanajitokeza wajanja wachache wenye nia ovu wanaofanya upotoshaji.

Ndani ya chama tawala asijitokeze mmoja akajiita ana uzalendo sana kuliko wenzake na kupata umaarufu wa kipinzani, huyo ana yake na ni kwa mahitaji yake wala hana alama ya uzalendo.

Tulipofika kama Taifa waambata wa vinara wa ufisadi wanajiita wazalendo na hata waliokuwa marafiki zao kwa kuwa wamebadili njia eti nao wanajiita wafia nchi.

Tumefika mahali ambapo, waliokuwa wanasimamia misingi ya Serikali na utekelezaji wa majukumu yake miezi kadhaa iliyopita, leo wakiwa pembeni wanatafuta njia murua ya kuendesha mapambano dhidi ya Serikali yao.

Hizi ni harakati na raha moja ya harakati unajificha kwenye mgongo wa kuwa mzalendo na kwa kuwa unaowaambia pengine hawajui tafsiri, unafikia mahali unajikuta umeaminiwa na kukubalika.

Watanzania na utaifa wetu

Misingi ya utaifa italindwa na sisi wenyewe. Tanzania ni Taifa huru lenye mipaka na katiba yake, lenye watu wenye mila na desturi tofauti. Watanzania tunaunganishwa na jambo moja – utaifa.

Tuna makabila tofauti na kwa msingi huo tunajenga tamaduni tofauti zenye mielekeo tofauti zaidi ya 150. Kwa hili, makabila yanabaki kuwa sehemu ya majigambo ya utani wetu, lakini sio jambo la maana hata kidogo.

Taifa letu bado ni maskini, na hata fikra zetu na uelekeo wa ubobezi wetu ni katika misingi hiyo ya umaskini.

Katika mapambano kisiasa bado tupo kwenye hatua za kusemea maisha ya wananchi maskini na hatujatoka kujielekeza kwenye ujenzi wa fikra pana.

Sauti na kelele zetu haziwezi kutoka kwenye kuzungumzia umaskini \wakati ili tupate nafasi tulizo nazo mtaji wetu tumeuweka kwa maskini.

Bahati mbaya hata zinapokuja juhudi za makusudi kupambana na umaskini, wanajitokeza miongoni mwa wapambanaji wanatetea wakandamizaji.

Sijui labda ni upofu tu, kwamba katika Tanzania hii wapo mabingwa wa kutetea mafisadi na wahujumu uchumi wetu. Wanashindwa kuwasikiliza akina mama maskini vijijini, vijana vijiweni wanaokubali kwa kauli moja kwamba njia pekee ya kuwaondoa wao katika mkandamizo ni vita vya kiuchumi.

Uaminifu wetu na mapenzi yetu miongoni mwa wanasiasa za harakati unatia shaka sana. Tunalo deni kama Taifa kujenga uchumi, misingi ya uzalendo, utii na uadilifu, kulinda amani na mshikamano pamoja na kupambana na rushwa za aina zote kwa maeneo yote.

Vinara wa ukosoaji

Napata wakati mgumu kuelezea hali ninayoiona Tanzania. Ni kama tuna watu wa mataifa mawili yenye kuhasimiana. Ni kama tuna watu wenye kutaka kuona machafuko lakini wanakosa sababu ya kuyatangaza. Ni wabinafsi, waongo na wajivuni. Ni vigeugeu na hawaoni kazi kuitakasa haramu kwa matakwa yao. Jambo baya linakuwa kwa wengine ni halali.

Sijui na sitakaa nijue tunashabikia nini. Ni katika Tanzania pekee uongo na majungu yanatembea kwa kasi hata kuaminiwa kuwa huo ndiyo ukweli.

Ni katika Tanzania ambako wananchi zaidi ya asilimia 60 wanaishi vijijini kwenye maisha halisi ya Mtanzania, lakini bado wapo wanaotaka kuaminisha kuwa kila Mtanzania ana ufahamu bora kwa maoni ya mitandaoni.

Ni Tanzania peke yake unamkuta mheshimiwa mbunge anajenga hoja kwa kutumia taarifa aliyoisoma Instagram, Twitter au Facebook. Hapa ndipo tunapopata shida ya namna baadhi ya waheshimiwa wanavyoweza kutumia taarifa mbalimbali kwa manufaa ya Taifa.

Hatusemi kuwa habari za mitandaoni zisiaminiwe, maana itakuwa sawa na kusema hata makala haya myapuuze, lakini tunachosema ni kwa namna gani taarifa gani zinaweza kutumiwa na nani kwa wakati gani na kwa sababu ipi.

Misingi ya uzalendo na utiifu

Tunaweza kushindwa kutofautisha mizizi ya uzalendo na utiifu lakini tunaweza kukubaliana mzalendo kwelikweli ni mtiifu na sio kila mtiifu ni mzalendo.

Utiifu hasa kwa Serikali ni namna bora ya kufundisha uzalendo kwa watoto na yeye awekezaye kwa watoto apanda mbegu njema.

Utii una miiko na misingi yake. Utii katika mazingira yasiyo na adabu hujenga unafiki na ni kwa misingi hii tunasema Taifa lilifika kiwango cha kukosa utii na adabu, mambo yaliyokuwa yanavunja uzalendo.

Rushwa, ubadhirifu, ufisadi na mengine ya aina hii yalianza kulijengea Taifa la matabaka yaliyojaa chuki. Tazama leo hii Tanzania mtu mmoja wa Serikali akitumbuliwa, kila mmoja ana maoni ya chuki. Iwe wale wanaounga mkono kutumbuliwa huko au wale wanaopinga. Wote ni chuki.

Tulifika mahali na tulikuwa tunatumbukia kwenye dimbwi la kutokuaminiana kabisa, ndiyo maana hata tunapopata mageuzi makubwa kabisa ya kimfumo na ya kinidhamu wapo wanaofurahia dhidi ya wanaopanguliwa na wanaochukia dhidi ya mpanguaji mkuu.

Sikatai ukosoaji dhidi ya Serikali, lakini kuna watu tunaweza kusema ni kama wendawazimu. Tumejizoesha vibaya kwamba hakuna jambo jema Serikali inaweza kufanya.

Ikiwa tulidhihaki mpango wa elimu bure, tukaenda mbele kudhihaki ununuzi wa ndege, tukasogea kudhihaki ujenzi wa reli, tunadhihaki udhibiti sekta ya madini, basi tuko tayari kupokea lolote kutoka kwa maadui zetu na wakifanikiwa kama Taifa tutasambaratika.

Tujiulize. Je, upinzani maana yake ni kupinga kila kinachofanywa na Serikali? Tabia za baadhi ya wanasiasa wetu kuna wakati unajiuliza, hivi wanawafundisha nini watoto?

Tukiacha washamiri tutakuja kujilaumu mbele kwa sababu ya kutokujidhibiti na mambo haya.

Majukumu makuu ya Serikali ni mawili, kulinda na kusimamia sheria, na usalama wa taifa na watu wake na pili kukusanya kodi.

Dhana ya usalama inakwenda mbali na ni jukumu la Serikali kuona watu wake wako salama katika nyanja zote na ili iweze kutekeleza hayo lazima ikusanye fedha nyingi za kutosha na chanzo kikuu ni kodi.

Serikali inayotekeleza majukumu ya msingi kwa wananchi wake inastahili kuheshimiwa na kusikilizwa.

Taifa limepiga hatua kubwa katika huduma za jamii yaani elimu, afya na maji. Changamoto hazikosekani, lakini kiwango cha utoaji huduma za afya leo ni bora mara 400 kuliko ilivyokuwa miaka minne iliyopita.

Sasa wananchi wana uhakika wa kupata dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali.

Serikali ya awamu ya tano sio ya mchezomchezo. Imefikia vigenzo kupewa utii, adabu na kuogopwa. Inalinda usalama wa Taifa, watu na mali zao licha ya changamoto zinazoikabili.

Inalinda na inajipambanua kuwa iko tayari kupoteza uhusiano na marafiki zake (mataifa ya nje) ili ilinde mali na amali za Taifa. Lakini kwa ushahidi wa wazi imejipambanua kuwa ni mkusanya kodi mkubwa.

Wakosoaji wamepambana sana, lakini Rais mwenyewe kama vile hasikii na hapo ndipo Watanzania sasa tunatembea kifua mbele kwa utaifa wetu.

Taifa limepata heshima, limepata kujulikana tena, tumerudi kwenye ile Tanzania ya ukombozi na sasa tupo katika vita ya ukombozi wa uchumi. Tulipambana na wakoloni waliotutesa na kutunyonya, wakaiba rasilimali zetu, wakajibebea kila walichotaka kwa misingi ya ukoloni, na leo bado tuendelee kuwavumilia wanaotuibia mali zetu kwa misingi ya sheria za kimataifa?

Je, unajua kuwa hata mkataba wa Berlin wa mwaka 1884-85 ulikuwa mkataba wa kimataifa? Kwa sababu za uzalendo, tunakubali na tutaridhia makosa kadha wa kadha yanayoweza kujitokeza, na kwa sababu ya utii tutayachukua kuwa ni ya kwetu. Ni afadhali Rais anavyoamua hata akikosea tutarekebisha makosa hayo.

Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka, siyo ya kuendeleza harakati. Najua wakosoaji hata makala hii hawataipenda lakini nitaisimamia nchi yangu hata kwa gharama ya utu wangu.

Falesy Kibassa ni msomaji wa magazeti ya Mwananchi, mtafiti na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya Kondoa.

Simu: +255716696265/barua pepe; [email protected]