Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

M/kiti UWT alivyowaliza waombolezaji mazishi dereva wa Heche

Muktasari:

  • Sweezy Maradufu alifariki dunia Julai Mosi, 2026 mkoani Kigoma.



Tarime. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisema chanzo cha kifo cha Sweezy Maradufu, aliyekuwa dereva wa Makamu Mwenyekiti wake, John Heche kitajulikana baada ya siku 28, simulizi ya maisha ya dereva huyo zimewaliza   mamia ya waombolezaji.

Sweezy Maradufu, alifariki dunia Julai Mosi, 2026 mkoani Kigoma. Mwili wake ulikutwa katika nyumba ya kulala wageni aliyokuwa amefikia. Amezikwa leo Julai 5, 2026 katika Mtaa wa Kekohogoma mjini Tarime, Mkoa wa Mara.

Salamu za rambirambi za baadhi ya wazungumzaji katika msiba huo, zimewapa waombolezaji wakati mgumu wa kudhibiti vilio, wengi walijikuta wakitoa vitambaa na kufuta machozi kila iliposimuliwa historia ya maisha ya duniani ya Maradufu.

Aliyewaliza wengi zaidi ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Mara, Nancy Msafiri, alipotoa salamu kwa niaba ya chama chake tawala.

Akizungumza msibani hapo, Nancy amesema Maradufu hakuwa na wazazi wala wakwe, hivyo yeye ndiye aliyesimama kama mbadala wa mzazi wake na mkwe wake.

Mwili wa Dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema taifa John Heche,  Sweezy Maradufu ukiwasili uwanjani kwaajili ya shughuli za mashi mjini Tarime.  Picha na Beldina Nyakeke

Licha ya mazingira hayo, amesema alimudu majukumu ya uzazi kiasi cha kuifanya familia hiyo kuwa bora na inayomcha Mungu.

Amemwelezea Maradufu kuwa mtu aliyeipenda kazi yake na alifanya kila namna kuhakikisha bosi wake anakuwa salama.

"Heche nakuomba usimuche Hawa (mke wa marehemu), Sweezy alikuwa mume, baba wa watoto wake na baba wa mke wake pia majukumu haya aliyamudu vema familia yake ilisimama vizuri,” amesema huku machozi yakionekana kwa waombolezaji ambao walikuwa wakishika vitambaa na kujifuta.

“Mimi naahidi kuchangia mifuko 25 ya saruji ili kukamilisha ule ujenzi wa nyumba yake," amesema Nancy ambaye baada kumaliza kutoa salamu hizo alikumbatiana na Heche, huku waombolezaji wakiangua vilio.


Kauli ya Chadema

Akizungumza kuhusu msimamo wa chama hicho kuhusu kifo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, amesema wana mashaka kihusu kifo hicho hivyo kimeamua kufanya uchunguzi wa kina wa kisayansi ili kubaini chanzo chake.

Amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kifo cha Maradufu kimetokana na kuziba kwa mshipa mkubwa unaopeleka damu kutoka kwenye moyo kwenda kichwani hali iliyosababisha shinikizo kubwa kutokana na damu kuganda.

Mwili wa Dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema taifa John Heche,  Sweezy Maradufu ukiwasili uwanjani kwaajili ya shughuli za mashi mjini Tarime.  Picha na Beldina Nyakeke

"Shinikizo lile lisingempa fursa ya kuendelea kuishi kwani damu iliganda, sasa tunataka kujua ukweli nini kilisababisha hali hii na uchunguzi huu tunataka ufanyike kisayansi," amesema.

Baada ya kufariki, amesema kucha za marehemu zilibadilika rangi na kuwa za bluu na  kulingana na maelezo ya wataalamu hali hiyo inaweza kusababishwa na kunyongwa au kula sumu.

Amesema baada ya uchunguzi huo wa awali walibaini kuwa kifo cha Maradufu hakikutokana na kunyongwa kwani baada ya kuchanwa shingoni hakuna mshipa ulikutwa ukiwa umedhurika wala kupasuka.

Kulingana na maelezo ya wataalamu, amesema upo uwezekano wa kifo hicho kusababishwa na sumu ambayo inaweza kuwa amekula kwenye chakula, kuvuta kwenye hewa au kufunikwa pua kwa kutumia kitambaa chenye sumu.

Kutokana na utata huo, amesema wameamua uchunguzi wa kisayansi ufanyike na sampuli muhimu za baadhi ya viungo vya marehemu zimechukuliwa na kupelekewa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

"Wakati wa kufungua sampuli hizo lazima kutakuwa na uwakilishi wa chama na familia, tunataka kuwa na uhakika na kifo hiki hadi sasa tunasema hiki kifo sio cha kawaida," amesema.

Golugwa pia, amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma kuomba radhi kwa familia na chama kutokana na kitendo cha askari polisi kusambaza picha ya baadhi ya vitu vya marehemu ikiwepo dawa zilizokutwa kwenye begi lake.

"Katika eneo la tukio hakuna mtu aliruhusiwa kupiga picha zaidi ya askari polisi mmoja lakini cha kushangaza zile picha zimesambazwa mitandaoni, tunamtaka RPC aombe radhi kwa kusambaza picha hizo kinyume cha sheria na taratibu," amesema.

Heche, amesema kifo hicho ni shambulio kubwa kwake na kwa chama chake pia huku akisisitiza sio cha kawaida.

"Mimi nadhani hiki kifo kilinilenga, Sweezy amekufa kwa niaba yangu na hii inatokana na ukweli kuwa alinipenda na kuwa mwaminifu sana kwangu. Alipitia mengi sana kwa ajili yangu ikiwa ni pamoja na kushambuliwa kwa kukatwa mapanga mwaka 1997 kwa ajili yangu," ameeleza

Amesema utata wa kifo hicho unatokana na sababu kadhaa ikiwemo kitendo cha kufuatiliwa na watu aliodai kuwa ni askari polisi ambao walikuwa wakitumia magari yaliyokuwa yanabadilishwa namba za usajili mara kwa mara huku wakiwa wamefunika nyuso zao.

"Tukiwa pale Makambako tulibaini watu walikuwa wanatufuatilia na waliendelea hivyo hadi tulipofika Tabora na waliendelea hivyo hadi mpakani mwa Tabora na Kigoma baadaye tuliamua kuwafuata na kuwauliza kwa nini wanatufuatilia walisema ni maofisa wa polisi. Tukawauliza kwa nini wanatufuatilia kimya kimya wakawa hawana majibu," amesema.

Heche amesema Maradufu hakuwa na historia ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukizwa licha ya kuwa na umri mkubwa jambo ambalo linazidi kuwapa imani kuwa kifo hicho sio cha kawaida.

"Juzi tulikuwa tunamtania kuwa Julai mosi anatimiza miaka 52 wakati akiwa hana changamoto yoyote ya kiafya akawa anasema yeye yuko imara kwa kweli kifo hiki kimeniachia simamzi kubwa sana.

“Sweezy nilimuamini sana nilikuwa nasinzia akiwa anaendesha gari jambo ambalo nilikuwa siwezi kufanya nikiwa na dereva mwingine," amesema.

Amesema alikuwa ni dereva mwenye nidhamu ya hali ya juu kiasi cha kushindwa kumiliki simu janja ili kuepuka kuchati wakati anaendesha gari na kwamba alipokuwa akiendesha gari hakuwa na tabia ya kupokea simu hata kama angepigiwa mara nyingi.

Akieleza mazingira ya kifo cha Maradufu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema taifa (Bavicha), Deogratius Mahinyila amesema waliukuta mwili wa marehemu ukiwa umelala kifudifudi sakafuni.

"Pengine alikuwa ameamka anakwenda kufanya shughuli zake, au alikuwa anatoka nje kutafuta hewa kama ambavyo inasemekana kuwa hewa ilipungua mle chumbani, lakini kikubwa ni kwamba Sweezy amekufa akipambania maisha yake," amesema.


Salamu za Chaumma, Matiko

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Butiku Mwita, amesema Serikali inapaswa kumuachia huru Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ili aendee na harakati zake za kutetea taifa.

"Taifa lina hitaji haki, tunataka Lissu awe huru aendeleze mapambano, vyama vya siasa viachwe vifanye siasa, Serikali isizuie mikutano ya vyama vya siasa, tunataka watu wapaze sauti kwa ajili ya haki ya kila Mtanzania," amesema

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema kifo kinapangwa na Mungu hivyo kila mmoja anapaswa kujiandaa kwani hakuna anayejua siku wala saa ya kuondoka kwake.

Amesema suala la majonzi na msiba kwa ujumla linapotokea linapaswa kuwaunganisha watu wote kwa pamoja bila kujali tofauti zao.

"Tumepoteza nguzo muhimu na mtu ambaye alikuwa ni msingi wa maendeleo ya Tarime yetu, ndio maana nimeamua kuja kuungana nanyi katika jambo hili gumu,wakati wa matatizo tunapaswa kuwa pamoja bila kuangalia na kujali tofauti zetu," amesema.

Mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Ester Matiko, amesema Maradufu alikuwa na utu, hekima na busara na kwamba kifo chake kimeacha pengo kwa familia na Chadema kwa ujumla.

"Nimekuwa familia ya Chadema kwa miaka 15, nimefanya naye kazi kwa karibu sana, alikuwa mtu mwema na ndio maana amefanya kazi na Makamu Mwenyekiti kwa muda wote huo hakuwa dereva tu bali alikuwa familia ya Heche," amesema.