Mwili wa dereva wa Heche wafanyiwa uchunguzi, sampuli kuchunguzwa zaidi kisayansi
Muktasari:
- Uchunguzi umefanywa na jopo la madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, wataalamu kutoka Wizara ya Afya Dodoma pamoja na ofisa kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Dar es Salaam. Mwili wa Suezi Maradufu, aliyekuwa dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche umefanyiwa uchunguzi wa kisayansi, huku sampuli zikichukuliwa kwa ajili ya vipimo zaidi kubaini chanzo halisi cha kifo chake.
Hatua hiyo imekuja baada ya Chadema kutaka uchunguzi huru ufanyike, kufuatia kifo cha Maradufu, aliyekutwa amefariki dunia ndani ya chumba cha nyumba ya kulala wageni mkoani Kigoma na kuzua maswali kutoka kwa viongozi na wanachama wa chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma iliyotolewa leo Ijumaa, Julai 3, 2026, uchunguzi huo umefanywa na jopo la madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC).
Pia, wapo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, wataalamu kutoka Wizara ya Afya Dodoma pamoja na Ofisa Mwandamizi kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Polisi wamesema uchunguzi huo umefanyika mbele ya viongozi wa Chadema na ndugu wa marehemu.
"Baada ya uchunguzi huo wa wataalamu hao wakishirikiana na Jeshi la Polisi, sampuli zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kisayansi ili kuthibitisha chanzo halisi cha kifo," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Maradufu amefariki dunia usiku wa kuamkia Julai mosi, 2026, ziarani mkoani Kigoma na mwili wake ulikutwa ndani ya chumba alichokuwa amepanga katika nyumba ya kulala wageni ya Ntahamba.
Julai 2, 2026 Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa aliiambia Mwananchi kuwa chama hicho kinataka kufanyika kwa uchunguzi wa kina ambao ungeshirikisha wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando na Wizara ya Afya, ili kuondoa sintofahamu kuhusu mazingira ya kifo hicho.
Jeneza lenye mwili wa Suezi Maradufu, aliyekuwa dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche.
Wakati Polisi wakitoa taarifa hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa amesema wataalamu wa afya wamefanya uchunguzi kwa kupasua kichwa na tumbo ili kubaini chanzo cha kifo kwa kuangalia viungo vinavyoonekana kwa macho.
"Katika hatua ya sasa, taarifa ya awali ya madaktari imedhibitisha kuwa hakuna jeraha la nje wala la ndani lililosababisha kifo chake. Hata hivyo, walibaini kuwa mshipa mkubwa unaopeleka damu kwenye ubongo ulikuwa umeganda, hali iliyosababisha shinikizo kubwa na hatimaye mauti yake," amesema Golugwa.
Amesema bado uchunguzi unaendelea kubaini kilichosababisha hali hiyo ya kuganda kwa damu, akisisitiza kuwa chama hicho bado kina mashaka kuhusu chanzo halisi cha kifo hicho.
Aidha, amesema sampuli mbalimbali zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa maabara ili kubaini iwapo marehemu alipewa sumu kwa njia ya kunywa, kula au kupuliziwa.
Kwa mujibu wa Golugwa, sampuli zilizochukuliwa ni kutoka kwenye machozi, pua, ubongo na figo kwa ajili ya vipimo zaidi.
Taarifa ya awali
Kwa mujibu wa Polisi, taarifa za awali kuhusiana na kifo hicho zilipokelewa Julai 1, 2026 kutoka kwa Mrimi Zabron Mwita, Katibu wa John Heche, aliyedai kuwa walifika nyumba ya kulala wageni kumwamsha Maradufu baada ya kumpigia simu mara kadhaa bila mafanikio, wakitaka kuendelea na ratiba yao ya safari.
Polisi wamesema walifika eneo la tukio wakiwa na Mrimi pamoja na wafanyakazi wa nyumba hiyo na kuonyeshwa chumba alichokuwa amelala marehemu.
Walieleza kuwa mlango wa chumba ulikuwa umefungwa kutoka ndani, hivyo walilazimika kuuvunja mbele ya mashuhuda.
Kulingana na taarifa ya Polisi, baada ya mlango kufunguliwa, walimkuta Maradufu akiwa amelala chini kifudifudi na kwa uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo, walibaini uwepo wa dawa mbalimbali za binadamu kwenye chumba alichokutwa marehemu.