Prime
Mapya kifo cha dereva wa Heche
Muktasari:
- Marudufu maarufu ‘Mzee Suez’ amezaliwa Julai mosi, 1974 Mkoani Mara na kufariki dunia Julai mosi, 2026 akiwa ziarani mkoani Kigoma.
Dar es Salaam. Kifo cha dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche Suez Maradufu, kimewaacha katika majonzi familia, viongozi na wanachama wa chama hicho, baada ya kufariki dunia tarehe ya kuzaliwa kwake.
Maradufu, maarufu kwa jina la ‘Mzee Suez’, alizaliwa Julai mosi, 1974 mkoani Mara na kufariki dunia leo Jumatano, Julai mosi, 2026 ziarani mkoani Kigoma. Mwili wake umekutwa ndani ya nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philimon Makungu akizungumza na Mwananchi leo kuhusiana na kifo hicho, amesema mwili wa Maradufu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni kwa ajili ya uchunguzi.
Taarifa za kifo hicho zilitolewa awali na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, aliyesema mwili wa Maradufu ulikutwa ukiwa umelala sakafuni karibu na mlango wa chumba alichokuwa amelala.
“Kwa masikitiko makubwa napenda kuwajulisha kifo cha dereva wa makamu mwenyekiti wetu, aliyefariki dunia leo asubuhi hapa Kigoma. Suez amekuwa dereva wa Heche kwa muda mrefu sana,” amesema Golugwa.
Amesema asubuhi ya leo, Heche pamoja na madereva wengine walimpigia simu bila mafanikio, ndipo walipoamua kwenda kwenye nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia.
“Tulipofika tulikuta mlango umefungwa. Tuliwajulisha polisi, ambao walifika na kuvunja mlango, ndipo wakaukuta mwili wa Suez ukiwa sakafuni,” amesema.
Kwa mujibu wa Golugwa, mwili wa marehemu umepelekwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku viongozi wa Chadema na mawakili wa chama hicho wakifuatilia taratibu zote zinazohusu tukio hilo.
Kamanda Makungu amesema uchunguzi wa awali unaonyesha Maradufu alikuwa akitekeleza majukumu yake hadi jana jioni.
“Jana jioni alikuwa anamwendesha Heche, baadaye akaenda kulala. Asubuhi alipogongewa mlango hakuamka. Hatuwezi kueleza kilichomsibu hadi uchunguzi wa madaktari ukamilike,” amesema.
Alipoulizwa iwapo kuna mtu yeyote anayehisiwa kuhusika na tukio hilo, Makungu amesema ni mapema kufikia hitimisho lolote, akisisitiza kuwa uchunguzi bado unaendelea.
Pia, amekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa Maradufu ameuawa.
“Wanaoeneza taarifa hizo watatusaidia katika uchunguzi kama kweli wana taarifa hizo. Tusubiri ripoti ya madaktari kabla ya kutoa hitimisho,” amesema.
Waliomfahamu wamzungumzia
Viongozi na wanachama wa Chadema wamemwelezea Maradufu kuwa mtu aliyekuwa na upendo, nidhamu na aliyejituma katika kazi yake.
Golugwa amesema Maradufu alianza kuwa dereva wa familia ya Heche tangu alipokuwa akimhudumia baba yake, kabla ya kuendelea kuwa dereva wa Heche aliposhinda ubunge mwaka 2015.
“Suez alianza kwa kumwendesha marehemu baba yake Heche. Baada ya Heche kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015, ndiye aliyekuwa dereva wake katika kampeni na akaendelea kuwa naye hadi sasa,” amesema.
Ameongeza kuwa hata baada ya Heche kutopata ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Maradufu aliendelea kuwa miongoni mwa wasaidizi wake wa karibu.
“Amekuwa sehemu ya familia ya Chadema kupitia kazi yake na Heche. Alikuwa mtu mtulivu, mwenye nidhamu, anayeheshimu muda na aliyeipenda kazi yake,” amesema Golugwa.
Msaidizi wa Heche, Joseph Mrimi amesema kifo hicho ni pigo kubwa kwao kutokana na mchango na uaminifu aliouonyesha kwa miaka mingi.
“Ilikuwa si rahisi mtu kulisogelea gari la Heche bila sababu. Alikuwa mwaminifu, mcheshi na mwenye kuwajali watu. Tumepoteza mtu muhimu na sasa tunasubiri matokeo ya uchunguzi ili mipango ya mazishi ianze,” amesema.
Naye kada wa Chadema, Hilda Newton kupitia ukurasa wake wa Facebook, ameandika Maradufu alikuwa mtu mwenye upendo na aliyegusa maisha ya wengi waliomfahamu.
“Nimekufahamu kupitia Heche. Ulikuwa mtu mwenye upendo mwingi, baba na rafiki wa kila aliyebahatika kukufahamu. Kifo chako kimetuachia simanzi kubwa. Pole kwa familia na pole kwa Heche kwa kumpoteza dereva wake,” ameandika Hilda.