Hii hapa bei mpya ya mafuta, petrol na dizeli zashuka
Muktasari:
- Bei kikomo za mafuta zitakazotumika Julai mwaka huu zinaonyesha kuwa, mafuta ya petroli yaliyopitia bandari ya Dar es Salaam yamepungua kwa Sh96, dizeli kwa Sh151 na mafuta ya taa kwa Sh242.
Dar es Salaam. Watuamiaji wa bidhaa za mafuta wanaanza kupata ahueni na kiasi cha fedha wanachotumia mafuta kikipungua kufuatia kupungua kwa bei Julai.
Bei kikomo za mafuta zitakazotumika Julai mwaka huu zinaonesha, petroli inayopitia bandari ya Dar es Salaam imepungua kwa Sh96, dizeli kwa Sh151 na mafuta ya taa kwa Sh242.
Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) iliyotangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zitakazotumika kuanzia leo Jumatano ya Julai Mosi, 2026.
Kupungua kwa bei hiyo sasa itafanya petroli ndani ya Dar es Salaam, lita moja kununuliwa kwa Sh3,990 kutoka Sh4,086 iliyokuwa ikitumika Juni mwaka huu, huku Dizeli ikinunuliwa kwa Sh4,182 kutoka Sh4,333.
Upande wa watumiaji wa mafuta ya taa yanayopitia bandari hiyo watanunua lita moja kwa Sh4,443 kutoka Sh4,685 iliyokuwa ikitumika Juni mwaka huu.
Kwa upande wa watumiaji wa mafuta yanayopitia bandari ya Tanga, sasa watanunua lita moja ya petroli kwa Sh4,051 ikiwa ni pungufu kutoka Sh4,157 huku dizeli ikinunuliwa kwa Sh4,243 kutoka Sh4,404 iliyokuwapo mwezi uliotangulia.
Upande wa mafuta ya taa watanunua lita moja kwa Sh4,504 kutoka Sh4,756 iliyokuwa ikitumika mwezi uliotangulia.
Wakazi wa Mtwara na mikoa jirani wanaotumia mafuta yanayopitia kusini mwa Tanzania, wao watanunua lita moja ya petroli kwa Sh4,083 ikiwa ni pungufu kutoka Sh4,193 huku dizeli ikinunuliwa kwa Sh4,275 ikilinganishwa na Sh4,440 iliyokuwapo Juni na mafuta ya taa yakifikia Sh4,536 kutoka Sh7,792.
Kupungua huku kwa bei za mafuta kunatajwa kuchangiwa na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Marekani na Iran kuhusu vita inayoendelea eneo la Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kuruhusu meli za mafuta kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz, ambapo bei za mafuta katika soko la dunia zimeanza kushuka.
Hilo limeenda sambamba na juhudi zinazofanywa na kampuni zinazosafisha mafuta ghafi kuendelea kutafuta na kununua zaidi kutoka katika maeneo yasiyo na vita ili kuwa na uhakika wa kupata bidhaa hiyo na kuendelea kusafirisha na kusambaza duniani kote.
Juni 26, 2026, bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha nishati hiyo inakuwapo wakati wote lakini bei yake inapungua pia. Aligusia kuhusu ahueni hiyo itaanza kuonekana kwa bei za Julai.
Hata hivyo, wastani wa bei hizo bado haujapungua kufikia kiwango kilichokuwepo kabla ya kuanza kwa vita hiyo Februari 28, 2026.
Kufuatia hali hiyo, Ewura imezitaka kampuni za mafuta kuwa huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa.
Bei hizo ni kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa Januari 28, 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 57 na marekebisho ya Kanuni tajwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 761A la Oktoba 30, 2023 na Mabadiliko ya Kanuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja za Mwaka 2024.
“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
"Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani,” imeeleza taarifa hiyo ya Ewura iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, Gerald Maganga.
Maganga amesema ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja, huku adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni.
“Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita,” ameeleza.
Stakabadhi hizo zitatumika kama ushahidi kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko kikomo au kuuziwa yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa.
“Pia stakabadhi hizo zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli,” amesema.