Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahueni bei ya mafuta kushuka yaanza kuyeyuka

Muktasari:

  • Ongezeko la bei ya mafuta limeshuhudiwa kuanzia Machi 2026, baada ya kuzuka kwa vita Mashariki ya Kati vilivyohusisha Marekani, Israel na Iran.

Dar es Salaam. Matumaini ya dunia kurejea katika hali ya utulivu na gharama za maisha kupungua yanaendelea kufifia baada ya kurejea kwa mapigano kati ya Marekani na Iran, huku pande hizo zikiendelea kushutumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa.

Miongoni mwa athari zilizojitokeza kutokana na mapigano hayo ni kupanda kwa bei ya mafuta duniani, ikiwemo Tanzania, misukosuko katika masoko ya fedha, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na athari kwa usafiri wa anga.

Wiki iliyopita, Marekani na Iran zilifikia makubaliano yaliyolenga kupunguza mvutano wa kijeshi, kusitisha mapigano na kuimarisha usalama katika eneo la Ghuba.

Hata hivyo, tangu yalipotangazwa, kumekuwa na taarifa zinazokinzana kutoka kwa viongozi wa nchi hizo kuhusu iwapo makubaliano hayo yameanza kutekelezwa kikamilifu.

Makubaliano hayo yenye vipengele 14 yalijumuisha kufunguliwa kwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz, pamoja na kuzuia Iran kumiliki silaha za nyuklia.

Hormuz hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayouzwa duniani. Kufungwa au kutishiwa kwa njia hiyo kulisababisha hofu ya upungufu wa mafuta, hali iliyochochea kupanda kwa bei za nishati na bidhaa mbalimbali duniani.

Mkataba huo ulisainiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, miezi minne baada ya kuanza kwa mzozo uliowahusisha Marekani, Israel na Iran.

Licha ya kutiwa saini, makubaliano hayo yaliibua wasiwasi kutokana na kutogusa kwa kina baadhi ya masuala muhimu yaliyopewa uzito na Iran, jambo lililoibua mashaka kuhusu uimara wake.

Hali imeanza kuwa tete baada ya Iran kudai kushambulia miundombinu ya kijeshi ya Marekani katika kambi mbili zilizopo Kuwait na Bahrain, ikisema ilikuwa inalipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vitano vya pwani vya Iran.

Serikali za Bahrain na Kuwait zimethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo, huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait ikiyalaani vikali na kuyataja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na BBC Swahili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imezituhumu Marekani kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kusisitiza kuwa Tehran ina haki ya kulinda mamlaka yake na uhuru wa kujitawala.

"Marekani haijawahi kuheshimu ahadi zake," ilisema sehemu ya taarifa ya Iran.

Saa chache kabla ya mashambulizi hayo, Rais Trump alisema jeshi la Marekani lilishambulia maghala ya makombora, ndege zisizo na rubani na vituo vya rada vya Iran, akidai operesheni hiyo ilikuwa jibu la kile alichokiita ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Trump pia alionya kuwa iwapo Marekani italazimika kuongeza nguvu za kijeshi, Iran itakabiliwa na madhara makubwa zaidi.

Kwa upande wake, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilisema lilitekeleza mashambulizi dhidi ya vituo muhimu vya kijeshi vya Marekani, vikiwemo Kambi ya Anga ya Ali Al Salem nchini Kuwait na makao makuu ya Jeshi la Wanamaji la Marekani la Fifth Fleet nchini Bahrain, kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.

IRGC ilidai ililenga vituo vinane vya kijeshi vya Marekani, ikisema hatua hiyo ilikuwa jibu la mashambulizi ya awali yaliyofanywa na Washington dhidi ya vituo vya Iran kwa kile ilichokiita kisingizio cha kulinda usalama wa usafiri wa baharini katika Mlango wa Hormuz.

Hata hivyo, hadi sasa maofisa wa Marekani hawajatoa taarifa kuhusu kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi hayo wala kuthibitisha iwapo kuna watu waliojeruhiwa au kupoteza maisha.

Hofu kuhusu usalama wa nishati imeendelea kuwapo, huku mashambulizi hayo yakisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa miundombinu katika maeneo yaliyohusika, na baadhi ya wananchi wakilazimika kuhama makazi yao.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa kutoka Chuo cha Diplomasia, Denis Konga, amesema kinachoendelea kinaonesha unafiki wa Marekani, akieleza kuwa ilikuwa vigumu kwa taifa hilo kufikia makubaliano na Iran huku likimkingia kifua mshirika wake wa karibu, Israel.

"Kuendelea kwa vita hii ni hatari kwa dunia. Kwanza, bei za nishati zitaendelea kupanda. Ingawa kulikuwa na matarajio kwamba kuanzia mwezi ujao zingeshuka, hali hiyo haiwezi kutokea," amesema.

Amesema kutokana na hali hiyo, dunia itaendelea kushuhudia mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali, ikiwemo mbolea, ambayo kwa kiasi kikubwa huagizwa kutoka nje ya nchi.

Juni 26, 2026, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, akizungumza bungeni jijini Dodoma, alionesha ahueni ya kushuka kwa bei ya mafuta kuanzia mwezi ujao, huku ndani ya wiki nane hadi 10 bei hizo zikitarajiwa kushuka duniani kote.

Ndejembi alisema kuanzia Julai mwaka huu wananchi watashuhudia bei ya mafuta ikishuka nchini, huku duniani kote ikitarajiwa kushuka ndani ya wiki nane hadi 10.

Alisema pamoja na kupanda kwa bei ya nishati hiyo, haikuwahi kukosekana nchini na hata gharama yake ni ndogo ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Kwa kuwa kuna makubaliano ya kusitisha mapigano Mashariki ya Kati, alisema bei ya mafuta imeshuka na kufikia dola 70, hivyo mamlaka nchini zinapaswa kuhakikisha ahueni hiyo inawagusa wananchi.

Alisema hadi sasa kuna meli zinaendelea kupakua mafuta na nyingine ziko njiani kuja Tanzania, hivyo wananchi wasiwe na hofu kwani uhaba wa nishati hiyo hautatokea tena.