Mtoto wa Museveni aibua mapya, afungia vyombo vya habari Uganda
Muktasari:
- Hatua hiyo imetangazwa kupitia ujumbe wa Muhoozi katika mtandao wa X, ambapo amesema NTV Uganda na Daily Monitor zinafungwa kuanzia leo na kusisitiza kuwa hazitaruhusiwa kurejea kufanya kazi bila idhini yake.
Kampala. Mvutano kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Majeshi, Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kuagiza kufungwa kwa shughuli za kampuni kubwa ya habari ya Nation Media Group (NMG), inayomiliki gazeti la Daily Monitor, kituo cha televisheni cha NTV Uganda pamoja na redio na vyombo vingine vya habari.
Hatua hiyo imetangazwa kupitia ujumbe wa Muhoozi katika mtandao wa X, ambapo amesema NTV Uganda na Daily Monitor zinafungwa kuanzia leo na kusisitiza hazitaruhusiwa kurejea kufanya kazi bila idhini yake.
Muda mfupi baadaye, Daily Monitor ilitangaza kupitia ukurasa wake wa X ofisi zake zilizopo jijini Kampala zilikuwa zimezingirwa na wanajeshi wenye silaha, huku walinzi wa jeshi wakidhibiti eneo hilo. Kwa mujibu wa The Daily Star.
Mbali na Daily Monitor na NTV Uganda, vyombo vingine vinavyomilikiwa na Nation Media Group vikiwemo Dembe FM, KFM, Spark TV na The East African navyo viliripotiwa kuathiriwa na hatua hiyo.
Katika ujumbe mwingine, Muhoozi amesema haamini kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda, akisisitiza kuwa vyombo hivyo vinapaswa kuongozwa kwa kufuata misingi.
"Kuanzia sasa vyombo vyote vya habari nchini Uganda vitalazimika kufuata sheria," ameongeza.
Hatua hiyo imeibua wasiwasi kuhusu hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda, ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikikosolewa na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.
Muhoozi Kainerugaba ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, ambaye ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986. Mara kadhaa amekuwa akivuta hisia za umma kutokana na matamshi yake makali kupitia mitandao ya kijamii kuhusu masuala ya kisiasa na kijeshi.
Hadi taarifa hii inaandaliwa, serikali ya Uganda bado haijatoa tamko rasmi kueleza msingi wa hatua hiyo wala muda ambao vyombo hivyo vitabaki vimefungwa.