Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jamhuri ilivyojibu mapigo pingamizi la Lissu

Muktasari:

  • Jamhuri ilifungua shauri hilo la maombi ya mapitio Februari 24, 2026, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam kuikatalia maombi yake ya kutaka iruhusiwe kuwasilisha ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa huyo



Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama ya Rufani imuamuru Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumlipa fidia kwa madai ya kuchelewesha usikilizwaji wa kesi yake na kumfanya aendelee kusota mahabusu.

Jamhuri ilifungua shauri hilo la maombi ya mapitio Februari 24, 2026, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam kuikatalia maombi yake ya kutaka iruhusiwe kuwasilisha ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa huyo.

Shauri hilo la mapitio namba 7203216/2026 limesikilizwa leo Ijumaa, Julai 3, 2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Zainabu Muruke na Amour Khamis, sambamba na pingamizi lake dhidi ya shauri hilo.

Katika pingamizi hilo, amedai uamuzi huo wa Mahakama Kuu hauwezi kukatiwa rufaa wala maombi ya marejeo kwa kuwa ni aina ya uamuzi ambao haumalizi kesi ya msingi.


Majibu ya Jamhuri

Akijibu hoja hizo kwa niaba ya jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amesema kifungu cha 8 (2) (d) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa (AJA), alichokitumia Lissu kuwasilisha pingamizi lake kinatumika kwa mashauri ya madai.

Amedai maombi yao yamefunguliwa chini ya kifungu cha 6(3) AJA na kanuni ya 65 ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za Mwaka 2009 na kwamba katika maombi yao hakuna mahali ambako wanaiomba Mahakama kupitia uamuzi bali maelezo ya Mahakama kuukataa ushahidi huo.

Wakili Katuga amedai kifungu hicho walichokitumia kinaipa mamlaka Mahakama ya Rufani kuitisha na kupitia mwenendo wa shauri la Mahakama Kuu ili kujiridhisha na uhalali na usahihi wa amri au uamuzi wowote.

Wakili Katuga amesisitiza kifungu cha 8(2) (d) cha AJA, kinazungumzia Mahakama kukataa kukata rufaa au mapitio ya amri au uamuzi na jambo ambalo si wao wanalolilalamikia.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema amedai kwa mujibu wa kanuni ya 107 ya Kanuni za Mahakama ya Rufani pingamizi la awali lazima liwe na uwezo wa kuondoa shauri la msingi.

Amedai kwamba, pingamizi lililowasilishwa na Lissu halina uwezo wa kuyaondoa maombi hayo, hivyo halina msingi.

Amesisitiza kifungu cha 8(2) (d) kinazuia rufaa na mapitio au uamuzi usiomaliza shauri kwenye mashauri ya madai na kwamba shauri lililoko mahakamani si shauri la madai.

Akijibu hoja hizo za Jamhuri, Lissu amesisitiza kinacholalamikiwa na Jamhuri kwa mujibu wa maombi hayo ni uamuzi ambao umejadili ushahidi waliotaka kuuingiza na Mahakama ikaangalia sheria ikasema kuwa ushahidi unaoombwa kuingizwa ni kinyume cha sheria na ikaukataa.

Lissu amedai kifungu cha 6 cha AJA kina vifungu vidogo vingi na kwamba ingawa Wakili Katuga kwa mdomo amesema kuwa wamefungua maombi hayo chini ya kifungu cha 6(3), lakini kwa kuangalia maombi yenyewe hakuna mahali ambako wametaja kifungu cha 6(2) au 6(3).

Hata hivyo, amedai kifungu cha 6(3) cha AJA kinaipa mamlaka ya kiusimamizi Mahakama yenyewe baada ya mdaawa kuandika barua ya malalamiko lakini hakimpi mdaawa mamlaka ya kuiomba Mahakama kufanya mapitio.

Hivyo amedai Jamhuri ilipaswa kuwasilisha maombi hayo chini ya kifungu cha 6(2) cha AJA, lakini akasisitiza kuwa bado pia angeiwekea pingamizi chini ya kifungu cha 8(2) (d) kwa kuwa uamuzi huo haukatiwi rufaa wala kufanyiwa mapitio.

"Kwa hiyo hawana hoja na rufaa (mapitio) haya hayana msingi kabisa. Wanataka kuipoka Mahakama mamlaka yake," amesema Lissu.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote imeahirisha shauri hilo mpaka itakapotoa uamuzi wake kwa tarehe ambayo wadaawa watajulishwa.

Jaji Mwarija amesema kama watakubaliana na pingamizi la Lissu basi uamuzi utaishia hapo kwenye pingamizi na kwamba kama katika uamuzi huo pingamizi hilo litakataliwa basi wataendelea kutoa uamuzi wa maombi ya msingi.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.


Katika maneno hayo Lissu alitamka kuwa:-

"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli...kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko...kwa hiyo tunaenda kikinukisha...sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana..."

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa Jamhuri na tayari mashahidi 15 wameshatoa ushahidi.

Februari 18, 2026 Jamhuri iliwasilisha mahakamani kwa njia ya mtandao, notisi ya kuongeza ushahidi katika kesi hiyo chini ya kifungu 308(1) cha CPA, ambayo ilisikilizwa Februari 23, 2026.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga ameileza Mahakama katika notisi hiyo wanaomba kuongeza ushahidi wa ziada katika ushahidi wa Kamishna Msaizidi wa Polisi (ACP) Amin Mahamba.

Hata hivyo, Lissu alipinga maombi hayo akidai kuwa 308(1) cha CPA (kilichotumiwa na Jamhuri) kinazungumzia shahidi ambaye maelezo yake hayakusomwa katika mwenendo kabidhi na si ushahidi mpya ambao haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.

Alieleza ushahidi wa Mahamba ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi, hivyo mlango wake wa kuleta ushahidi mpya umeshafungwa.

Pia alidai ushahidi huo unaobishaniwa hauwezi kutumika kwa kosa analotuhumiwa kwani lilifanyika Aprili 3, 2025, akashtakiwa Aprili 10, 2025 na kupelekwa mahabusu, lakini ushahidi huo wa nyongeza ni wa kabla na baada ya uchaguzi.

Mahakama katika uamuzi wake Februari 24, 2026 ilikubaliana na hoja za Lissu kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 308 CPA, maelezo au ushahidi unaotolewa notisi unapaswa uwe ule ambao wakati wa mwenendo kabidhi ulikuwepo lakini haukusomwa na si ambao haukuwepo.

Jaji Ndunguru alisema notisi hiyo ililenga kuwasilisha ushahidi uliopatikana baada ya mwenendo kabidhi. Hivyo Mahakama iliikataa notisi hiyo ikisema inakwenda kinyume na kifungu cha 308 cha CPA, ndipo Jamhuri ikafungua shauri hilo la mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu.