Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu, Jamhuri kupimana tena ubavu kisheria mahakamani leo

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wakati akitoka katika kizimba cha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam Jumatano, Februari 18, 2026 baada ya kesi yake kuahirishwa. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini inayosikilizwa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam. Jamhuri imefungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuikatalia kuwasilisha ushahidi mpya, ambalo limepangwa kusikilizwa leo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo kwa mara nyingine anatarajiwa kuchuana na jopo la mawakili wa Serikali kwa hoja za kisheria wakati wa usikilizwaji wa shauri lililofunguliwa dhidi yake na Jamhuri, kuhusiana na kesi ya uhaini inayomkabili.

Jamhuri ilifungua shauri hilo la maombi ya mapitio Februari 24, 2026, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, kuikatalia maombi yake ya kutaka iruhusiwe kuwasilisha ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa huyo.

Shauri hilo la mapitio namba 7203216/2026 limepangwa kusikilizwa leo, Ijumaa, Julai 3, 2026, na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani litakaloketi Dar es Salaam, linaloongozwa na Jaji Augustine Mwarija. Majaji wengine ni Zainabu Muruke na Amour Khamis.

Awali, kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani vya usikilizaji wa mashauri, shauri hilo la mapitio lilikuwa limepangwa kusikilizwa Juni 11, 2026, lakini usikilizwaji huo ulisogezwa mbele mpaka leo, na hakuna sababu za mabadiliko hayo zilizowahi kuwekwa wazi.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Inadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi aliwashawishi wananchi kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Katika maneno hayo Lissu alitamka kuwa:

"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli... kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko... kwa hiyo tunaenda kukinukisha... sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kweli kweli... tunaenda kukinukisha vibaya sana..."

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, likiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde, iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa Jamhuri, na tayari mashahidi 15 wameshatoa ushahidi.

Februari 23, 2026, upande wa mashtaka kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ulieleza mahakamani kuwa Februari 18, 2026 uliwasilisha kwa njia ya mtandao notisi ya kuongeza ushahidi katika kesi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 308(1) cha CPA.

Wakili Katuga alisema katika notisi hiyo wanaomba kuongeza ushahidi mpya katika ushahidi wa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Amin Mahamba kwani haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.

Alisema notisi hiyo imeambatanishwa na kiini cha ushahidi huo, akifafanua kuwa ACP Mahamba alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wakati wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi, na kwamba walitambua ushahidi huo Februari 16, 2026 wakati wakimuandaa shahidi huyo.

Hata hivyo, Lissu alipinga maombi hayo akidai kifungu cha 308(1) cha CPA (kilichotumiwa na Jamhuri) kinazungumzia shahidi ambaye maelezo yake hayakusomwa katika mwenendo kabidhi na si ushahidi mpya ambao haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.

Akijibu hoja hizo, Wakili Katuga alidai kifungu cha 308(1) cha CPA kinazungumzia notisi ya shahidi mpya au ushahidi wake ambao haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi.

Lissu alisisitiza kuwa kifungu cha 308 cha CPA kinazungumzia shahidi mpya na si ushahidi mpya, na kwamba shahidi mpya ni yule ambaye maelezo au ushahidi wake haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.

Alieleza kuwa ushahidi wa ACP Mahamba ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi, hivyo mlango wa kuleta ushahidi mpya kupitia ushahidi wake umeshafungwa, na kwamba hatua ya kuongeza ushahidi mpya kwa ushahidi wake ambao umeshasomwa kwenye mwenendo kabidhi ni kutaka kubadilisha hati ya mashtaka.

"Waheshimiwa majaji, mlango wa Amin Mahamba ulishafungwa kwenye committal (mwenendo kabidhi), na kama Jamhuri wanataka maelezo hayo yazungumzwe, basi wamtafute shahidi mwingine ayazungumzie na siyo Amin Mahamba," alidai Lissu.

Kuhusu kiini cha ushahidi huo unaobishaniwa, Lissu alieleza kosa analotuhumiwa lilifanyika Aprili 3, 2025, akashtakiwa Aprili 10, 2025 na kupelekwa mahabusu, lakini maelezo hayo ya nyongeza yanahusu kipindi cha kabla na baada ya uchaguzi.

Mahakama katika uamuzi wake wa Februari 24, 2026 ilikubaliana na hoja za Lissu kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 308 cha CPA, maelezo au ushahidi unaotolewa kwa notisi unapaswa kuwa ule ambao wakati wa mwenendo kabidhi ulikuwepo lakini haukusomwa, na si ule ambao haukuwepo.

"Kwa hiyo kifungu cha 308 kinafungua mlango kwa shahidi ambaye maelezo yake yalikuwepo lakini hayakusomwa, lakini hakifungui mlango wa kuleta ushahidi ambao haukuwepo au ushahidi ambao umeletwa baadaye," alisema Jaji Ndunguru.

Alisema notisi hiyo ililenga kuwasilisha ushahidi uliopatikana baada ya mwenendo kabidhi, yaani baada ya uchaguzi, hivyo ni dhahiri kwamba wakati mwenendo kabidhi unafanyika ushahidi huo haukuwepo. Hivyo, alisema notisi hiyo inakwenda kinyume na kifungu cha 308 cha CPA.

"Hivyo mahakama inakubaliana na pingamizi lililoletwa kwamba notisi hii haiendani na kifungu cha sheria, na hivyo tiba pekee ni mahakama kuitupilia mbali. Kwa hayo, mahakama inaitupilia mbali notisi hii," alisema Jaji Ndunguru.

Baada ya uamuzi huo, ndipo upande wa mashtaka ukakimbilia Mahakama ya Rufani ambako ulifungua shauri la mapitio ya uamuzi huo, na hivyo Mahakama Kuu ikalazimika kusimamisha usikilizaji wa kesi ya msingi kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika shauri hilo.