Usikilizwaji maombi ya Jamhuri dhidi ya Lissu wasogezwa mbele
Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wakati akitoka katika kizimba cha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam Jumatano, Februari 18, 2026 baada ya kesi yake kuahirishwa. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Mwenyekiti huyo wa Chadema anakabiliwa na kesi ya uhaini inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imesogeza mbele tarehe ya usikilizaji shauri la maombi ya mapitio lililofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, kwa siku 21 zaidi.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani vya usikilizaji mashauri (cause list) ambayo Mwananchi liliiona nakala yake Ijumaa Mei 29, 2026, shauri hilo la mapitio namba 7203216/2026 lilikuwa limepangwa kusikilizwa kesho Alhamisi Juni 11, 2026.
Hata hivyo habari zilizopatikana leo Jumatano, Juni 10, 2026 siku moja kabla ya tarehe hiyo iliyokuwa imepangwa awali zinaeleza kuwa sasa shauri hilo litasikilizwa Julai 3, 2026.
“Ni kweli kuna mabadiliko hayo ya tarehe. Kwa mujibu wa hati ya wito wa mahakama tuliyoipokea sisi inaonesha sasa shauri litasikilizwa Julai 3, 2026,” amesema mmoja wa waendesha mashtaka wa kesi hiyo kuthibitisha mabadiliko hayo ya tarehe ya usikilizwaji wa shauri.
Naye mwanasheria mkuu wa Chadema ambaye pia ni miongoni mwa mawakili wanaomsaidia Lissu katika kufanya utafiti wa hoja mbalimbali za kisheria wakati kesi hiyo inasikilizwa, Dk Rugemeleza Nshala amethibitisha kupata taarifa za mabadiliko ya tarehe hiyo ya usikilizwaji wa shauri hilo.
Hata hivyo, hakuna sababu zozote ambazo zimeshafahamika kuhusiana na mabadiliko hayo.
Shauri hilo limepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani litakaloketi Dar es Salaam, linaloongozwa na Jaji Augustine Mwarija. Majaji wengine katika jopo hilo ni Zainabu Muruke na Amour Khamis.
Jamhuri ilifungua shauri hilo mahakamani hapo Februari 24, 2026, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kuikatalia kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa huyo, hatua ambayo ilifanya kesi ya msingi kusimama kusikilizwa.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli...kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko...kwa hiyo tunaenda kikinukisha...sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli... tunaenda kukinukisha vibaya sana..."
Kesi hiyo ya uhaini inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa Jamhuri na tayari mashahidi 15 wameshatoa ushahidi.
Jinsi ilivyokuwa
Februari 23, 2026, upande wa mashtaka kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga ulieleza Mahakama Februari 18, 2026 uliwasilisha mahakamani kwa njia ya mtandao, notisi ya kuongeza ushahidi katika kesi hiyo chini ya kwa mujibu wa kifungu 308(1) cha CPA.
Wakili Katuga alisema kuwa katika notisi hiyo wanaomba kuongeza ushahidi mpya katika ushahidi wa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Amin Mahamba kwani haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi (committal proceedings), kwenye mahakama ya ukabidhi (committal court), Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.
Alisema kuwa notisi hiyo imeambatanishwa na kiini cha ushahidi huo, akifafanua ACP Mahamba alikuwa ni kiongozi wa timu ya upelelezi wakati uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi na kwamba walitambua ushahidi huo Februari 16, 2026 wakati wakimuandaa shahidi huyo.
Lissu alipinga maombi hayo akidai 308(1) cha CPA (kilichotumiwa na Jamhuri) kinazungumzia shahidi ambaye maelezo yake hayakusomwa katika mwenendo kabidhi na si ushahidi mpya ambao haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Akijibu hoja hizo, Wakili Katuga alidai kifungu cha 308(1) cha CPA kinazungumzia notisi hiyo ya shahidi mpya au ushahidi wake ambao haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi.
Hata hivyo, Lissu alisisitiza kifungu 308 cha CPA, kinazungumzia shahidi mpya na si ushahidi mpya na kwamba shahidi mpya ni yule ambaye maelezo au ushahidi wake haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Alieleza ushahidi wa ACP Mahamba ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi, hivyo mlango wake wa kuleta ushahidi mpya umeshafungwa na kwamba hatua ya kuongeza ushahidi mpya kwa ushahidi wake ambao umeshasomwa kwenye mwenendo kabidhi ni kutaka kubadilisha hati ya mashtaka.
"Waheshimiwa majaji, mlango wa Amin Mahamba, ulishafungwa kwenye commital (mwenendo kabidhi) na kama Jamhuri wanataka maelezo hayo yazungumzwe basi wamtafute shahidi mwingine azungumzie na sio Amin Mahamba," alidai Lissu na kusisitiza:
"Kifungu 308 kinaelekeza maelezo ya shahidi mpya ndio yanayoweza kukubaliwa, lakini kwa ushahidi wa Mahamba milango yake imefungwa na kama ukikubaliwa madhara yake ni kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka."
Kuhusu kiini cha ushahidi huo unaobishaniwa Lissu alieleza kuwa kosa analotuhumiwa lilifanyika Aprili 3, 2025, akashtakiwa Aprili 10, 2025 na kupelekwa mahabusu, lakini maelezo hayo ya nyongeza yanahusu kabla na baada ya uchaguzi.
Uamuzi wa Mahakama
Mahakama katika uamuzi wake Februari 24, 2026 ilikubaliana na hoja za Lissu kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 308 CPA, maelezo au ushahidi unaotolewa notisi unapaswa uwe ule ambao wakati wa mwenendo kabidhi ulikuwepo lakini haukusomwa na si ambao haukuwepo.
"Kwa hiyo kifungu cha 308 kinafungua milango kwa shahidi ambaye maelezo yake yalikuwepo hayakusomwa lakini hakifungui mlango wa kuleta ushahidi ambao haukuwepo au ushahidi ambao umeletwa baadaye," alisema Jaji Ndunguru.
Alisema notisi hii ililenga kuwasilisha ushahidi uliopatikana baada ya mwenendo kabidhi, baada ya uchaguzi hivyo ni dhahiri kwamba wakati mwenendo kabidhi unafanyika ushahidi huu haukuwepo, hivyo alisema kuwa notisi hiyo inakwenda kinyume na kifungu cha 308 cha CPA.
"Hivyo mahakama inakubaliana na pingamizi lililoletwa kwamba notisi hii haiendani na kifungu cha sheria na hivyo tiba pekee ni mahakama kuitupilia mbali notisi hii,” alisema Jaji Ndunguru.
Baada ya uamuzi huo kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude aliomba ahirisho la muda wa saa moja kutafakari uamuzi huo kabla ya kuendelea, huku akifafanua kuwa wanahitaji muda wa kumuandaa shahidi mambo ya kueleza kwa kuzingatia uamuzi huo.
Waliporejea baada ya muda wa saa tatu ndipo Wakili Mkunde akaiarifu Mahakama hiyo kuwa DPP amefungua shauri la maombi ya mapitio dhidi ya uamuzi huo.
Kutokana na hatua hiyo Mahakama Kuu kwa mujibu wa sheria ililazimika kusimamisha mwenendo wa kesi hiyo kwa muda usiojulikana kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika shauri hilo la mapitio.