Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilio cha mtoto wa Lissu Bunge la Marekani chaibua mapya



Dar es Salaam. Ushuhuda wa Augustino Lissu, mtoto wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu mbele ya maofisa wa Bunge la Seneti na Congress nchini Marekani umeibua mjadala mpana nchini.

Wakati baadhi wakiona hatua hiyo kama njia ya kuwasilisha hoja za wananchi katika majukwaa ya kimataifa, wengine wameeleza athari zake kwa taswira ya Tanzania na mahusiano yake na washirika wa maendeleo.

Kijana wa Lisssu katika ushuhuda wake alieleza namna familia yao ilivyotenganishwa na kumfanya ashindwe kufurahi pamoja na baba yake.

Augustino amezungumza na maofisa hao Juni 5, 2026, Washington D.C, si kama mwanasiasa, bali kama mtoto aliyeishi sehemu kubwa ya maisha yake akimwona baba yake akiteseka kutokana na mapambano ya kisiasa na kupigania haki.

Alisema sehemu ya maisha yake imejengwa na kumbukumbu za majeraha ambayo baba yake aliyapata baada ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017 akibainisha ambavyo maisha ya familia yao yamekuwa yakikatizwa mara kwa mara na uhamisho, kutengana na vipindi vya kutokuwa pamoja kutokana na changamoto zinazomkabili baba yake mara kwa mara.

Hatua hiyo imeibua mjadala ambao kwa nyakati tofauti jana Jumapili Juni 7, 2026 baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema kilichofanywa na mtoto wa Lissu ni katika kuweka mashinikizo na kuongeza nguvu katika kile ambacho kinamgusa mtu binafsi au familia kutokana na kinachoendelea kwa mwanasiasa huyo.

Wamesema hali hiyo ina athari hasi kwa nchini, baadhi yao wakishauri aidha kesi hiyo kuendelea na kumalizika au Lissu aachiwe huru.

Profesa Mohammed Bakari amesema kilichofanywa na mtoto wa Lissu kina athari hasi kwa upande wa Serikali.

"Suala hili tayari limekuwa likizungumzwa na kuna muswada umepelekwa na wabunge wa Democratic na mwingine wa Republican, lakini mtoto wa kiongozi wa chama cha upinzani kueleza kwa mlengo si tu wa kisiasa bali kama familia kunachochea mwamko zaidi na kufanya shinikizo kuwa kubwa," amesema.

Amesema pamoja na kulegalega kwa demokrasia nchini, lakini haikuwahi kufika katika macho ya kidunia kwa kiasi kikubwa kama hivi sasa, licha ya kueleza kuwahi kutokea Zanzibar miaka ya nyuma.

"Hivi sasa inazungumzwa Tanzania, kilichofanywa na mtoto wa Lissu kinaweza kuchangia kuipa nguvu hata kesi iliyopelekwa mahakama ya kimataifa ya ukiukwaji wa haki za binadamu," amesema.

Amesema ili kupata muafaka ni nchini kukubaliana na ukweli na kutafuta suluhisho halisi kwani kilichoifikisha nchi hapo kinaeleweka.

Mchambuzi mwingine, Dk Paul Loisulie amesema suala la Lissu litaendelea kuibuka kwa namna mbalimbali kwa kuwa linavuta hisia na hivi sasa imekuwa la kidunia.

"Ambacho Serikali inapaswa kutambua ni kwamba hili suala haliwezi kupuuzwa, kitendo cha mtoto wake kutoa ushuhuda kimeleta hisia mpya.

"Taswira yake si nzuri, inaonekana kama Tanzania ni nchi ya mateso, watoto ndugu wa Lissu wanateseka," amesema.

Amesema ili kupata suluhu kuna mambo mawili, aidha kesi hiyo iendelee na ifike mwisho au aachiwe huru kwani si haki kuendelea kukaa mahabusu.

Dk Loisulie ameeleza historia ya matukio ya aina akigusia kesi ya aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

"Alikaa miezi minane mahabusu, si haba ni kesi ambayo ilivuta hisia za wengi, lakini alipotoka mambo yote yaliisha," amesema akibainisha namna ambavyo siasa ya Tanzania bado haijakubali mfumo wa vyama vingi kiuhalisia zaidi ya kwenye maandishi, akishauri litakapopita suala la Lissu nchi irekebishe aina ya siasa zake iwe ya vyama vingi kiuhalisia na viongozi wakubali kukosoana.

Naye Lugete Mussa amesema kwa alichokifanya mtoto wa Lissu ni kama familia ilishaona haina upepo  mzuri na Serikali, hivyo inajenga diplomasia ya kijamii nje ya nchi.

"Imeshafanikiwa kwenye Umoja wa Ulaya, mtoto wake alichokifanya juzi ni kuendelea kujenga mtandao nje ya mipaka na kujaribu kusukuma kete kwamba baba yao hana hatia.

"Labda wanadhani baba yao hatendewi haki na ukizingatia mazingira mengi ya wapinzani Afrika wanakutana na misukosuko kama ya Lissu, hata hivyo, tuiache Mahakama ni muhimili huru ufanye kazi yake," amesema.

Amesema mashinikizo ni mengi tangu mwaka 2017 Lissu alipopigwa risasi na athari kwa nchi zipo na si ajabu hiki kinachoendelea kinaweza kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia.

Septemba 7, 2017 Lissu alinusurika jaribio la mauaji kwa kupigwa risasi, miaka saba baadaye (Aprili 9, 2025) alikamatwa huko Mbinga mkoani Ruvuma akiwa katika mkutano wa hadhara akinadi msimamo wa Chadema kuhusu “No reforms, No election”, kaulimbiu iliyolenga kushinikiza mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi, alifunguliwa kesi ya uhaini na tangu wakati huo amekuwa gerezani kesi yake ikiendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.