Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bungeni bado kwa moto, kibano kipya kwa hawa chaja


Muktasari:

  • Baadhi ya wabunge na mawaziri walionekana wakiwa Morocco walikokwenda kuangalia fainali ya mpira wa miguu kwa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyocheza na vijana wa umri huo wa Senegal.



Dodoma. Utoro wa wabunge bungeni, kusainiana na kusafiri pasipo kupewa vibali, vimemuibua Spika Mussa Zungu akionya tabia hiyo huku akimwagiza Katibu wa Bunge kuwaandikia barua baadhi ya waliosafiri kwenda Morocco.

Pia, amemuomba Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuacha kutoa vibali kwa mawaziri na manaibu wao wa wizara moja kuondoka bungeni kwenda ziarani badala yake lazima mmoja wao abaki kufuatilia mijadala.

Zungu ambaye pia ni mbunge wa Ilala (CCM) jijini Dar es Salaam, ametoa agizo hilo jana bungeni Dodoma kwa Katibu wa Bunge, Baraka Leonard akitaka wabunge waliokwenda Morocco wajieleze ndani ya siku nne.

Baadhi ya wabunge na mawaziri walionekana wakiwa Morocco walikokwenda kuangalia  fainali ya mpira wa miguu kwa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyocheza na vijana wa umri huo wa Senegal.

Mechi hiyo ilichezwa usiku wa Juni 2, 2026 katika Uwanja wa Prince Moulay Hassan, Rabat na vijana wa Senegal kuibuka na ushindi wa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza baadhi ya wabunge na mawaziri walionekana wakiwa nje ya uwanja wakati wa mchezo jambo linalotajwa kama hawakuwa wamekwenda kwa lengo hilo badala yake huenda walikuwa na mambo yao.

Baada ya kipindi cha maswali, Zungu amesema tabia ya utoro ndani ya Bunge imekithiri.

“Katibu nakuagiza uwaandikie barua mara moja wabunge ambao walisafiri kwenda Morocco bila kibali cha Spika wajieleze na majibu yao yafije ndani ya siku nne kuanzia leo,” amesema Zungu.

Kiongozi huyo wa mhimili wa Bunge ametaja tabia ya utoro kwa wabunge imekuwa katika mitindo tofauti, ikiwamo wengine kusainiana ili kuonesha kama mhusika alishiriki vikao wakati siyo kweli.

“Kuna tabia imezuka siku hivi, mbunge haji bungeni lakini anamtuma mwenzake kuja kumsainia, hii siyo tabia njema, kuanzia sasa tutaanza kufuatilia na tunao mfumo wa kutambua nani hakuja na nani alimsainia, wote wawili wataingia hatiani,” amesema Zungu.

Kingine Spika amebainisha baadhi ya wabunge wamekuwa wakiomba vibali katika ofisi yake wanakwenda majimboni na kupewa, lakini kinyume chake wanasafiri kwenda nje ya nchi kitu alichosema ni hatari.

Amesema upo mfumo wa ufuatiliaji unaoweza kubaini mhusika kama yupo jimboni au nje ya nchi na hata nchi aliko inaweza kujulikana hata mhusika akiwa amezima simu.

Spika amemuomba Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki kusaidia katika jambo hilo, akisema kila kitu ni lazima kiende kwa utaratibu na kufuata kanuni.

Amesema inatia aibu kwa Bunge na hata wapigakura wakiona mwakilishi hayupo bungeni huku kukiwa hakuna sababu za msingi ingawa wengine hawaonekani bungeni bila taarifa lakini wanakuwa jijini Dodoma.

"Lakini mawaziri nao wanaondoka wote, najua wana vibali vyao lakini Waziri Mkuu, hawa wasipewe vibali vya ziara wote, akitoka waziri, naibu wake awepo bungeni siyo wanakosekana wote," amesema Zangu.

Kabla ya Zungu kueleza hayo, Dk Mwigulu aliposimama eneo la kujibu swali, alianza kwa kutoa agizo kwa wabunge na mawaziri kuhakikisha Juni 11, 2026 wanakuwepo wakati Serikali itakaposoma bajeti yake kwa mwaka 2026/27.

Mitazamo ya wadau

Mwananchi imezungumza na wadau mbalimbali kuhusu kile alichokieleza Spika Zungu kuhusu utoro.

Mbunge wa zamani,  Ferister Njawu amesema ni aibu kwa mbunge aliyeomba nafasi kwa wananchi halafu akaelezwa ni mtoro tena hahudhurii vikao.

Njawu amekiri japo utoro kwa wabunge ni wa siku nyingi, lakini akabainisha kwa mtu mwenye nia ya kuwasemea na kufikisha hoja za wananchi wake, lazima atakuwa mshiriki mwaminifu wa vikao vya Bunge kila wakati.

“Kuhusu hili la kwenda Morocco naona pia waliteleza lakini huenda jambo hili lilisukumwa na furaha ya kwenda kuwaona vijana wale wakicheza, hata hivyo sikubaliani na utamaduni aliosema Spika watu wanaomba ruhusa ya kwenda majimboni lakini ghafla wanasafiri nje, je mtu akipatwa na jambo lolote huko nje itakuwaje?” amehoji Njawu.

Wakili Godfrey Wasonga amesema udhaifu unaanzia kwenye kanuni ambazo hazimpi nafasi kubwa Spika ya kutoa uamuzi badala yake zimempa upande mmoja na kumpunguzia upande wa pili.

Wasonga amesema kanuni za Bunge na Katiba ya nchi zingepaswa kuwapa wananchi eneo pana la kuwawajibisha wabunge watoro badala ya kupeleka mambo hayo kwenye vyama vya siasa.

Mmoja wa watumishi wa Bunge ambaye hakupenda kutajwa majina yake, amesema Kanuni ya 167 ya Kanuni za Kudumu za Bunge zimetoa masharti ya namna gani mbunge anaweza kupewa kibali cha kusafiri au kuwa nje ya Bunge.

“Kwenye kanuni hiyo kifungu cha tano kimeandikwa, kwa madhumuni ya fasihi ya 4 ya kanuni hii, kibali kitatolewa katika ofisi za Bunge za Dodoma au Dar es Salaam au Zanzibar,” amesema.

Kwenye kifungu cha nne kinaeleza mbunge yeyote atayeshindwa kuhudhura vikao vya Bunge na kamati zake kwa sababu maalumu atatakiwa kupata kibali kwa Spika wakati kifungu cha tatu kinasema mbunge atakapokosa kuhudhuria nusu ya vikao vya mkutano mmoja bila sababu ya msingi atapewa onyo.

Hata hivyo, amesema katika uzoefu wake katika uzoefu wake tangu Bunge la tisa lililokuwa chini ya Spika Samuel Sita, ni Bunge hili la 13 ndilo limekuja na sura za utoro zaidi tena ikiwa ni kipindi cha mikutano ya mwanzo.