Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Kiti cha Spika kizuie mijadala ya aina ya ‘Yuda’, inazalisha chuki
Wiki iliyopita, Watanzania wamemshudia mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWZ), Simai Mohamed akilitumia Bunge kutoa tuhuma nzito za usaliti kwa mtu aliyembatiza jina la Yuda, nje kabisa ya mada iliyokuwa mezani.
Mimi nilitarajia, kiti cha Spika kingezuia aina hiyo ya mjadala ya kumshambulia mtu ambaye hakumtaja zaidi ya kusema yuko ndani ya Serikali na kuhoji kosa la mama yaani Rais Samia Suluhu Hassan ni nini hadi kiongozi huyo amsaliti.
Ukisoma Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo zimetungwa chini ya Ibara ya 89 ya Katiba, Kanuni ya 70(8) inayosimamia mbunge atalisemea tu jambo ambalo liko katika mjadala na Kanuni ya 73 inamtaka kusema ukweli na si jambo la kubuni.
Kwa hiyo nilitarajia kiti cha Spika kifanye mambo mawili, moja ni kumtaka mbunge huyo kuliambia Bunge, Yuda ni nani na pili atakiwe kuthibitisha kauli yake kwa sababu kanuni zinataka mbunge kuzungumzia jambo ambalo halina ukweli.
Ni kweli Kanuni ya 84(1) inasema mtu yeyote asiye mbunge, ambaye atajisikia kuwa amepata athari hasi kutokana na kauli au maneno ya shutuma, atapeleka malalamiko yake kwa Spika, lakini kwa suala hili jina la anayelengwa halijatajwa.
Bahati mbaya sana, ni kama Bunge lilikuwa limemwagiwa maji kwa sababu hakuna mbunge yeyote anayetokana na CCM aliyesimama kuomba mwongozo wa Spika au hata kusema kuhusu utaratibu ili Spika aweze kutoa mwelekeo sahihi.
Ni kweli Naibu Spika, Daniel Sillo aliingilia kati na kumtaka mbunge huyo kujadili mada iliyo mbele yake, lakini tayari damage (uharibifu) ilikuwa imeshafanyika.
Ingawa hakumtaja jina lakini kwa kuazima neno la kisheria la Innuendo ambalo linamaanisha kutomtaja mtu moja kwa moja (indirect), lakini kwa maudhui yake, mtu yeyote mwenye akili anajua aliyelengwa ni nani kama ilivyo katika suala hili.
Kabla sijachambua kauli yake hiyo, ni muhimu sana nikawarejesha katika kile ambacho mbunge Simai alikisema wakati akichambua hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha, ambapo aliibua tuhuma nzito dhidi ya msaidizi huyo wa Rais.
Simai alisema ndani ya Serikali kuna viongozi wasaliti aliowafananisha na Yuda na kusema: “Leo nambatiza mmoja aliyekuwepo ndani Serikali. Ni Yuda. Sisi tunataka maendeleo, kosa la mama ni wapi. Au ni kumuamini mtu kumbe ni Yuda.”
“Yuda huyu amesaliti ndugu zake hata ile familia ambayo ilimlea kisiasa. Hawataki kumuona huyu Yuda. Hata huko nyuma amewahi kutajwa ni mzigo lakini leo mzigo huu tunao ndani ya Serikali. Na hapa niseme ameshawaumiza watu wengi.”
“Wengine walikuwa mbele, sasa tunao huku nyuma back bench. Wapo wafanyabiashara, watendaji wa Serikali. Wengine ambao walikuwa na safari zao za kisiasa wamekatwa katwa wako nje na wameathirika na msongo wa mawazo.”
Akadai mtu huyo, ameibuka katika nyumba za ibada akitafuta huruma za watu na kutumia na kutumia majina ya viongozi wastaafu ili mradi aoneshe anapendwa.
Nikimnukuu zaidi, alisema: “Leo anapita akitaka kutuaminisha sisi sisi kwamba Rais Magufuli, alimpenda sana yeye Yuda. Kama alimpenda kweli mbona alimrusha huko nje ya dunia. Waliompenda hayati Magufuli wanajulikana na sasa wapo.”
“Yuda aache kutumia majina ya watu, tuamkeni wabunge na tusiogope. Siwezi kutia ulimi wangu puani. Maendeleo tunayoyataka lazima tuhakikishe Serikali inapata utulivu, mawaziri wanakuwa na amani na tunaacha kuchonganishwa.”
Hiyo ndio sehemu ya mchango wa mbunge huyo ambao umeachwa kubaki kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (hansard), kwamba anatoa tuhuma nzito hivi za usaliti kirahisi rahisi tu.
Ukitafakari na kuchambua kauli hii na matukio mbalimbali yaliyotokea kuanzia Rais Magufuli alipoingia madarakani na baadaye Samia, ni rahisi kujua anayelengwa ni nani, huyo anayemwagiwa upupu ni lazima awe ni mteule wa Rais.
Kwa muktadha huo, makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi ndiye msaidizi wa kwanza wa Rais na aliaminiwa na Samia akateuliwa kuwa mgombea Mwenza katika uchaguzi mkuu uliofanyia Oktoba 29, 2026, Je ndiye aliyelengwa?
Tunahoiji swali hili kwani ni Dk Nchimbi ndiye ambaye Desemba 3, 2016 aliteuliwa na Rais Magufuli kwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil lakini ndiye ambayo siku chache zilizopita alisoma ujumbe wa Rais Magufuli msibani.
Lakini ndiye ambaye Rais Samia amemuamini na kumteua kuwa Katibu mkuu wa CCM kabla ya kumteua kuwa mgombea mwenza wa Urais 2025.
Kama sio Nchimbi, ni nani sasa mwingine aliyekuwa analengwa? ni mteule gani wa Rais anayeshabihiana na sifa nilizozieleza isipokuwa Dk Nchimbi.
Lakini kwani wajibu wa mbunge anapokuwa bungeni ni upi?, anachangia mada zilizo mbele ya Bunge na kuwawakilisha wananchi waliomtuma (kwa wale wa kuchaguliwa), au anaweza kuongea lolote hata lisilo na masilahi kwa wapigakura.
Kama mbunge Simai hakuwa amemlenga Dk Nchimbi, basi kiti cha Spika kimtake amtaje mtu aliyemlenga na atoe uthibitisho kwa sababu tuhuma alizozitoa ni nzito na zina lengo la kumchonganisha na Rais, wana CCM na watanzania kwa ujumla.
Narudia kusema, kiti cha Spika kisipokuwa makini tunaweza kuwa na Bunge la hovyo kuwahi kutokea kwamba baadhi ya wabunge wanajadili mambo madogo madogo, utani mwingi, kejeli, mipasho badala ya kujikita kwenye ibara ya 63.
Ukisoma Ibara hiyo ya 63(2) ya Katiba inasema Bunge ndicho chombo kikuu hapa Tanzania ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri na vyombo vyake katika utekelezaji vyote wa majukumu yake.
Kazi za Bunge zilizoainishwa katika ibara hiyo ni pamoja na mbunge kumuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma na kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti kama ilivyo sasa.
Majukumu mengine ni kutunga sheria, kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa hapa Tanzania kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Tanzania ambayo inahitaji kuridhiwa.
Kwa hiyo Bunge ni eneo nyeti kweli kweli na inashangaza baadhi ya wabunge kutumia muda adhimu wa Bunge, tena wakilipwa vyema na pesa za kodi zetu, kupigana vijembe, kupongezana au kujibu hoja za wabunge badala ya Serikali.
Kiti cha Spika kikiwa makini, nina uhakika hata mbunge aliyeibua tuhuma nzito namna ile asingetumia hata dakika moja angeshakatishwa na mchango wake na kufutwa kwa sababu alimjadili mtu ambaye hamtaji wala hayuko bungeni.
Mchango wake umeibua taharuki kubwa mitaani kuwa pengine Rais Samia ambaye anaongoza nchi kwa sasa kuna mteule wake au msaidizi wake wa karibu anamhujumu, na nina uhakika akiambiwa athibitishe hilo hataweza.
Hivi tuseme ni kweli anachokisema, hivyo vyombo vyetu vya usalama ikiwamo Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ambayo sina shaka nayo hata kidogo, kwamba ingekuwa kimya na inatizama tu Rais akihujumiwa? Haiingii akilini hata kidogo.
Lakini, chama kinachotawala, kina vikao vyao vya kikatiba kuanzia Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) hawana taarifa juu ya msaidizi huyo wa Rais anayehujumu kazi nzuri za Rais Samia.
Kuna usemi unasema :“Whatever happens in politics, it is not by coincidence,” ukimaanisha "Chochote kinachotokea katika siasa, si kwa bahati mbaya,” hivyo ni wakati muafaka mbunge Simai awaeleze Watanzania ametumwa na nani?
Nina wasiwasi, Bunge lisipokuwa makini, linaweza kuingizwa katika migogoro ya kisiasa iliyo nje ya Bunge, na kujikuta linatumika kuchafua watu walio nje ya Bunge na ambao kwa asili ya kazi yao (nature), hawawezi kunyanyia mdomo kujitetea.
Bunge libaki kwenye msitari, ugomvi nje ya Bunge usiingizwe bungeni. Spika na Naibu Spika pamoja na wenyeviti wa Bunge simameni kwenye nafasi zetu.
Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) simama kwenye nafasi yako na wabunge wote kwa jumla wenu, simamieni utiifu wa kanuni za Bunge.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 065660090