Prime
Mtoto wa Lissu afikisha kilio cha familia Bunge la Marekani
Muktasari:
- Tundu Lissu ametimiza takribani miezi 14 tangu akamatwe Aprili 9, 2025. Sasa mwanaye, Augustino Lissu amefikisha kilio cha familia mbele ya maofisa wa Seneti na Congress ya Marekani.
Dar es Salaam. Augustino Lissu, mtoto wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ametoa ushuhuda wake mbele ya maofisa wa Bunge la Seneti na Congress nchini Marekani, akieleza namna familia yao ilivyotenganishwa na kumfanya ashindwe kufurahi pamoja na baba yake.
Simulizi ya kijana huyo ameeleza kwamba familia ya Lissu, ambaye ametimiza zaidi ya mwaka mmoja gerezani huku kesi yake ikiendelea mahakamani, imebeba vilio vya mashambulizi, uhamisho, vifungo na utengano wa familia hiyo.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 huko Mbinga mkoani Ruvuma akiwa katika mkutano wa hadhara akinadi msimamo wa Chadema kuhusu “No reforms, No election”, kaulimbiu iliyolenga kushinikiza mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.
Mwanasiasa huyo ambaye alinusuri jaribio la mauaji kwa kupigwa risasi Septemba 7, 2017, alifunguliwa kesi ya uhaini na tangu wakati huo amekuwa gerezani wakati kesi yake ikiendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Augustino amezungumza na maofisa hao Juni 5, 2026, Washington D.C, si kama mwanasiasa, bali kama mtoto aliyeishi sehemu kubwa ya maisha yake akimwona baba yake akiteseka kutokana na mapambano ya kisiasa na kupigania haki.
Katika simulizi yake iliyosambazwa mitandaoni, imewagusa wengi waliohudhuria, kwa mujibu wa mwanaharakati na mwanamitindo wa Tanzania anayeishi Marekani, Tausi Likokola, akisema baadhi ya waliokuwa ukumbini walishindwa kujizuia kutoa machozi waliposikia simulizi ya kijana huyo.
Alichokisema Augustino
Akizungumza na maofisa hao, kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa mitandaoni, Augustino amesema sehemu ya maisha yake imejengwa na kumbukumbu za majeraha ambayo baba yake aliyapata baada ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017.
“Kamwe sikupata nafasi ya kucheza michezo ya kawaida ya kurushiana mpira na baba yangu kwa sababu mkono wake haukuweza kunyooka tena kikamilifu. Ninachojua ni kwamba katika maisha yake yote ya utu uzima, amepigania kile alichoamini ni sahihi na ameendelea kuadhibiwa kwa sababu hiyo,” amesema.
Kwa mujibu wa Augustino, maisha ya familia yao yamekuwa yakikatizwa mara kwa mara na uhamisho, kutengana na vipindi vya kutokuwa pamoja kutokana na changamoto zinazomkabili baba yake mara kwa mara.
Amesema hali hiyo imeifanya familia yao kuendelea kuishi katika mazingira ya kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake.
Wakati huohuo, viongozi na wanachama wa Chadema, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho John Heche, wamekuwa wakisisitiza kuwa kukosekana kwa mwenyekiti wao kumekiweka chama katika mazingira magumu ya kisiasa na kiutendaji.
Akisimulia mazungumzo ya Augustino kupitia ukurasa wake wa Instagram, Tausi Likokola, amesema simulizi ya Augustino mbele ya maofisa wa Marekani ilimgusa zaidi katika safari yake ya utetezi wa haki za binadamu.
Likokola amesema alikuwapo pamoja na mwanawe ambaye pia ni mwanafunzi wa sayansi ya siasa, jambo lililomfanya aone kwa karibu maumivu ya mtoto anayekua huku baba yake akiwa gerezani.
“Tunaendelea kudai kuachiwa kwa Tundu Lissu na kupatikana kwa haki kwa wote wanaoshikiliwa, waliopotezwa, wanaoteswa au wanaolengwa kwa sababu ya kusema ukweli wao,” amesema katika taarifa yake.
Hoja ya Maseneta Marekani
Ziara ya Augustino imejiri wakati kukiwa na shinikizo la maseneta wawili wa Marekani, Jeanne Shaheen na Ted Cruz, waliowasilisha muswada bungeni wakitaka kufanyika upya kwa tathmini katika uhusiano wa Marekani na Tanzania.
Wabunge hao wanapendekeza kuiwekea vikwazo Tanzania kutokana na kile wanachokiita ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanyika nchini.
Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni pamoja na vizuizi vya viza kwa viongozi na wanasiasa, tathmini upya ya ushirikiano wa kiusalama na mapitio ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia.
Hatua hiyo, ililiibua Bunge la Tanzania ambapo wabunge waliitaka Serikali ya Tanzania kutumia njia za kidiplomasia kuzungumza na maseneta wa Marekani ili kumaliza sintofahamu hiyo.
Walisisitiza juu ya umuhimu wa kuheshimu uhusiano na ushirikiano mwema na mataifa ya nje kwa kujali na kulinda uhuru na mamlaka ya nchi.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania inaamini katika diplomasia ya mazungumzo kama njia kuu ya kumaliza tofauti zinazoibuka.
Balozi Kombo alisema tayari wamemwelekeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dk Elsie Sia Kanza kufanyia kazi hoja za maseneta hao.
Pia, Balozi Kombo alisema kiutaratibu hoja zilizotolewa maseneta hao ndani ya Bunge lao zinatakiwa zijibiwe na wabunge wa Tanzania kama ilivyofanyika.