Sintofahamu mtoto atoweka katika mazingira tatanishi
Muktasari:
- Kwa siku 20 sasa, familia yake inapitia kipindi kigumu cha majonzi na sintofahamu. Kila siku inayopita huongeza maswali kuhusu hatima ya mtoto huyo.
Mtwara. Hofu, wasiwasi na maswali yasiyo na majibu vimetanda katika Mtaa wa Pachoto A, Kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani, kutokana na kupotea kwa mtoto, Bidhat Salumu (10).
Bidhat, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Naliendele, hajulikani alipo tangu Juni 15, 2026 alipoenda kuuza maandazi, shughuli ambayo alikuwa akiifanya kila siku.
Kwa siku 20 sasa, familia yake inapitia kipindi kigumu cha wasiwasi na sintofahamu. Kila siku inayopita huongeza maswali kuhusu hatima ya mtoto huyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Pachoto A, Ismail Bakari, anasema walipokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo siku hiyo hiyo na kuanza jitihada za kumtafuta.
Anasema walifanya msako wa nyumba kwa nyumba na kutoa taarifa kwa wakazi wa maeneo jirani ili kusaidia kumpata mtoto huyo.
Baadaye taarifa hizo ziliwasilishwa kwa mtendaji wa mtaa, mtendaji wa kata na polisi kata ili kuongeza nguvu katika jitihada za utafutaji.
“Ni tukio la kwanza la aina hii kutokea tangu nianze kuongoza mtaa huu,” anasema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amethibitisha kupokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo na kuwa sasa uchunguzi unaendelea.
Anasema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na wananchi katika kufuatilia taarifa mbalimbali zinazoweza kusaidia kumpata mtoto huyo na kumrejesha kwa familia yake.
Pia, anawataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola pamoja na kuongeza uangalizi kwa watoto wao, ili kuzuia matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wao.
Pichani ni Bidhat Salum, mtoto anayetafutwa baada ya kupotea katika mazingira ambayo bado hayajafahamika.
Wakati uchunguzi ukiendelea, familia ya Salum inaendelea kuishi kwa wasiwasi na hofu. Kila siku wanaamka wakiamini huenda leo ndiyo siku ambayo simu italia na kuwaletea habari njema za kurejea binti yao akiwa nyumbani salama.
Mwananchi imefika nyumbani kwa familia hiyo na kuzungumza na wazazi, walezi, majirani na viongozi wa eneo hilo ili kufahamu kilichotokea.
Bibi asimulia siku ya mwisho
Bibi wa mtoto huyo, Asia Katoto amesema mjukuu wake alikuwa akimsaidia kuuza maandazi, machungwa na kashata za ufuta wakati wa likizo.
Anasema siku ya tukio, mtoto huyo aliondoka nyumbani na kuelekea katika Chuo cha Kilimo MAT-Naliendele ambako familia hiyo imekuwa ikifanya biashara zake ndogondogo.
“Kabla hajaondoka, nilimwambia arudi mapema nyumbani. Alinijibu vizuri kama kawaida na akaondoka,” anasema.
Asia, anasema wasiwasi ulianza baada ya saa kadhaa kupita bila kumuona akirejea nyumbani.
“Nilipoona muda unaenda na mtoto hafiki nyumbani, nilienda mwenyewe chuoni kuulizia. Nikaambiwa alishaondoka muda mrefu. Hapo ndipo hofu ilipoanza kuongezeka,” anasema.
Baada ya jitihada za awali kushindikana, familia ilianza kuwapigia simu ndugu na marafiki, lakini hakuna aliyekuwa amemwona mtoto huyo.
Hatimaye walitoa taarifa kwa viongozi wa mtaa, polisi jamii, kituo cha polisi na vyombo vya habari vya jamii, wakiamini huenda taarifa hizo zingesaidia kumpata.
“Hadi leo sijamuona mjukuu wangu. Naiomba Serikali na wananchi waendelee kutusaidia katika jitihada za kumtafuta,” anasema.
Mama mzazi
Mama mzazi wa Bidhat, Asia Mmahuta (30), anasema hakuwa nyumbani siku ya tukio kwa kuwa alikuwa shambani akifanya shughuli za kilimo.
Anasema alipokea simu iliyomjulisha kuwa bintiye alikuwa amepotea tangu asubuhi alipokwenda kuuza maandazi.
“Nilipata mshtuko mkubwa. Nilirudi nyumbani haraka na kuanza kushiriki kumtafuta mwanangu. Tangu siku hiyo tumekuwa tukimtafuta kila mahali bila mafanikio,” anasema.
Asia, anasema Bidhat ni mtoto wake wa kwanza na alikuwa ameweka matumaini makubwa kwake.
Anasema familia imefika katika mamlaka mbalimbali, ikiwamo Jeshi la Polisi na viongozi wa eneo, lakini bado hawajapata taarifa yoyote kuhusu alipo mtoto huyo.
Pamoja na maumivu anayopitia, anasema hajapoteza matumaini ya kumuona mwanawe akiwa hai na salama.
“Naendelea kumuomba Mungu. Kuna nyakati nakata tamaa, lakini bado naamini siku moja mwanangu atapatikana,” anasema.
Kwa sauti iliyojaa huzuni, mama huyo anasema jambo linalomuumiza zaidi ni kutofahamu hali ya mtoto wake.
“Leo ni siku ya 20. Sijui anakula nini, analala wapi au anapitia hali gani. Hayo ndiyo mawazo yanayoniumiza kila siku.”
Anasema Bidhat alikuwa sehemu muhimu ya maisha yake ya kila siku na mara nyingi alimsaidia kazi mbalimbali za nyumbani pamoja na kuwasaidia wadogo zake.
“Maumivu ya kumpoteza mwanangu hayaelezeki kwa maneno. Ni mtoto niliyembeba tumboni, nikamzaa na kumlea kwa taabu. Sitachoka kumtafuta,” anasema.
Tuhuma za ushirikina
Kadiri siku zinavyoendelea kupita bila taarifa za kupatikana kwa mtoto huyo, baadhi ya wananchi wameanza kutoa nadharia mbalimbali kuhusu tukio hilo.
Miongoni mwa madai yanayoenezwa ni kuhusisha tukio hilo na imani za kishirikina zinazodaiwa kujitokeza nyakati za msimu wa korosho.
Hata hivyo, bibi wa mtoto huyo, anasema madai hayo yameongeza maumivu kwa familia badala ya kuwasaidia.
“Tunapitia kipindi kigumu sana. Mbali na kumpoteza mtoto, tunalazimika kujibu tuhuma ambazo hazina msingi wowote,” anasema.
Asia Katoto, anasema nyumba wanayoishi imejengwa kwa mapato ya kilimo cha korosho na si kwa njia yoyote haramu.
Mama amtetea bibi
Kwa upande wake, mama mzazi wa Bidhat anasema haamini kabisa madai yanayomhusisha mama yake na kupotea kwa mtoto huyo.
Anasema amelelewa na mama huyo na kushuhudia namna alivyowalea watoto na wajukuu wengine wengi kwa upendo.
“Nilimuacha mwanangu kwa imani kubwa. Hata baada ya tukio hili, sijawahi kumshuku yeyote kwa sababu sijawahi kuona jambo lolote linaloweza kunifanya nifanye hivyo,” anasema.
Majirani waeleza hofu
Majirani wa familia hiyo wanasema tukio hilo limewaacha katika hofu kubwa na kuwafanya wazazi wengi kuongeza uangalizi kwa watoto wao.
Amina Mwalimu, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, anasema kupotea kwa Bidhat kumewashtua wengi kwa sababu ni mtoto waliyezoea kumuona kila siku.
“Tulishiriki kumtafuta lakini hadi sasa hakuna taarifa zozote. Ni tukio ambalo limetuumiza na kutuacha na maswali mengi,” anasema.
Anasema wakazi wa eneo hilo wanaendelea kumuombea mtoto huyo apatikane akiwa salama na kurejea kwa familia yake.