Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yatozwa faini ya Sh100 milioni kutumia 'Jumba la Maajabu'

Muktasari:

  • TPLB imesema adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu vyombo vya maamuzi.

Dar es Salaam. Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeitoza Klabu ya Yanga, faini ya Sh100 milioni baada ya kubainika kuwa wachezaji na benchi la ufundi walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja badala ya chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB iliyotolewa leo Julai 3, 2026, adhabu hiyo inatokana na ukiukwaji wa Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mechi, baada ya tukio hilo kutokea katika mchezo namba 233 uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, ambapo Yanga ilishinda mabao 3-0.

TPLB imesema adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu vyombo vya maamuzi.

Mbali na faini hiyo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imewapeleka kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Rais wa Yanga, Hersi Said na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine, kwa tuhuma za kutoa maelezo yanayodaiwa kuwa ya msingi usiokubalika na makosa ya kujirudia kuhusu matumizi ya vyumba rasmi vya kuvalia.

Jumba iliyo nje ya uwanja waliyotumia Yanga badala ya chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania.

TPLB imeeleza kuwa si mara ya kwanza kwa Yanga kuadhibiwa kwa kosa hilo, ikikumbusha kuwa mwezi Mei mwaka huu klabu hiyo ilitozwa faini ya Sh30 milioni kwa ukiukwaji wa kanuni hiyo hiyo baada ya kutumia nyumba iliyo nje ya uwanja badala ya chumba rasmi cha kuvalia.

Mara ya kwanza, Yanga ilifanya kosa hilo katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Simba ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Aidha, adhabu hiyo inakuja ikiwa Yanga imemaliza msimu wa 2025/26 kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya pointi 82, ikiwatangulia watani wao Simba waliomaliza nafasi ya pili.

Ubingwa huo ni wa tano mfululizo kwa klabu hiyo, ukiendeleza ubabe wake kwenye soka la Tanzania Bara.