Vibe kama lote la Tigo Fiesta, Fursa kuanzia Morogoro

Muktasari:

Msimu wa sikukuu kwa mashabiki wa Bongo Fleva nchini, Huu ni wakati wa Tamasha la Tigo Fiesta linaloanza kutimua vumbi leo Morogoro.

Ni msimu wa sikukuu kwa mashabiki wa Bongo Fleva nchini. Ndicho kipindi pekee wanachopata nafasi ya kukutana na wasanii wawapendao wakiwa pamoja. Huu ni wakati wa Tamasha la Tigo Fiesta linaloanza kutimua vumbi leo.

Huu pia ni msimu wa shamrashamra za kitamaduni katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Hii inafuatia uzinduzi mkubwa wa makubaliano kati ya Tigo Tanzania na Clouds Entertainment Group.

Wakitangaza makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga aliahidi kuwa tamasha la mwaka huu lililobeba kauli mbiu ya Vibe kama lote litakuwa kubwa na la kusisimua zaidi katika historia ya miaka 17.

‘Kauli mbiu ya Tigo Fiesta 2017 ni Vibe Kama Lote, ikionyesha sifa kuu kama mtandao unaoelewa zaidi mahitaji ya wateja wake nchini kote,’ anasema Mpinga.

“Ushirikiano huu unamaanisha kuwa pamoja na kuwa mtandao unaoongoza kwa mageuzi ya kidigitali nchini, Tigo kwa sasa pia ndio mtandao unaosisimua zaidi nchini. Tutawaletea wasanii wenye hadhi ya kimataifa na waliojizolea sifa ndani na nje ya nchi katika msimu wa miezi mitatu iliyojaa ofa kabambe kutoka Tigo zitakazoendana na shamrashamra za furaha na kumbukumbu za muziki.

Naye Katibu Mkuu wa Kamati ya maandalizi, Gardner G Habash alisema katika historia ya miaka 17, Tigo Fiesta imekuwa jukwaa la kukuza muziki wa nyumbani.

“Inawapa fursa wasanii kuonyesha uwezo wao na kuongeza idadi ya mashabiki ndani na nje ya nchi. Kuna maelfu ya mashabiki wanaohudhuria matamasha yenyewe au kufuatilia matukio kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,” alisema.

Mbali na kutoa burudani ya uhakika, Tigo Fiesta 2018 –Vibe Kama Lote pia itaibua fursa nyingi za kujiongezea kipato kwa wasanii pamoja na wakazi wa maeneo mbalimbali yatakayoshuhudia shamrashamra za msimu huu.

Pia katika msimu huu wa burudani, Tigo inatoa tiketi za watu mashuhuri (VIP) za kuhudhuria Tigo Fiesta 2018 kwa wateja ambao watanunua vifurushi vya Tigo VIP Pack ambavyo vinawapa wateja huduma bora zaidi za sauti, SMS na data kuanzia Sh30,000.

Vile vile, wateja wote wa Tigo pia watapata nafasi ya kujishindia zawadi kemkem kama vile pesa taslim na simu janja kwa kushiriki katika shindano la Tigo Fiesta Chemsha Bongo ambapo watatakiwa kujibu maswali yanayohusu Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote.

Gardner ameongeza kuwa msimu huu wa Vibe Kama Lote utajumuisha miji ya Morogoro, Sumbawanga, Iringa, Singida, Songea, Mtwara, Moshi, Tanga, Muleba, Kahama, Mwanza, Musoma, Arusha na Dodoma na Dar es Salaam.

Kuhusu Fursa

Huu ni mwaka wa sita kwa semina hizi za kufanyika toka imeanza. Hii imelenga zaidi kwa vijana kutambua na kuzitafutia suluhisho changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kujiletea maendeleo kwenye maeneo yao.

Kupitia fursa zilizopita tayari kuna matunda ya baadhi ya watu waliowahi kukata tamaa ambao kwa sasa wameanzisha biashara zao na wamekua wakichangia pato la Taifa kwa kulipa kodi.