Takukuru yawashikilia vigogo wawili wa NCU

Muktasari:

Wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhujumu mali za ushirika


Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inawashikilia kwa mahojiano vigogo wakuu wawili wa Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU), kwa tuhuma za kuhujumu mali za ushirika.

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Suzan Mwendu akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Aprili 20 amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa NCU, Jacob Shibiliti na makamu wake, John Magulu.

 Amesema kwa pamoja, waliokuwa viongozi hao wanadaiwa kufanya hujuma kwa kuuza mali za ushiriki zenye thamani ya zaidi ya Sh426.4 milioni kinyume cha sheria.

Kaimu kamanda huyo ametaja mali iliyouzwa kuwa ni kiwanja cha NCU kilichoko eneo la viwanda Igogo jijini Mwanza.

Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.