Vyuo 10 vya ualimu vyakarabatiwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Ukarabati umewanufaisha wanachuo wa Stashahada maalumu ya Sayansi, Hisabati na Tehama katika chuo cha Udom.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia Sh11.9 bilioni kukarabati miundombinu ya kufundishia, kujifunzia na mabweni katika vyuo 10 vya ualimu nchini.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Morogoro, Mpwapwa, Butimba, Kasulu, Songea, Tukuyu, Marangu, Kleruu, Korogwe na Tabora.

“Ukarabati huu umewezesha wanachuo 5,920 waliokuwa wanasoma Stashahada maalumu ya Sayansi, Hisabati na Tehama katika Chuo Kikuu cha Dodoma -Udom kuhamishiwa katika vyuo hivyo,” amesema.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Ijumaa, Novemba 17,2017 bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 11 ambalo limeahirishwa hadi Januari 30, 2018.

Amesema ili kuongeza fursa za wanafunzi kusomea ualimu, Serikali imepanga kujenga na kukarabati vyuo vya ualimu vya Kitangali, Ndala, Mpuguso na Shinyanga kwa thamani ya Sh36.47 bilioni. 

Waziri Mkuu Majaliwa amesema mradi huo ambao utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2016/17 hadi 2018/19, unalenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya ualimu.

“Ujenzi na ukarabati huu utasaidia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya Serikali kutoka wanachuo 20,535 katika mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 katika mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300,” amesema.

Wakati huohuo, waziri mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ukarabati wa vyuo saba vya ualimu vya Serikali.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Tandala, Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka, Patandi na Ilonga.

Amesema vyuo vya ualimu vya Murutunguru, Kabanga na Mhonda vitalazimika kujengwa upya baada ya wahandisi kubaini kuwa vyuo hivyo havifai kukarabatiwa kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake.