Waathirika wa Ukimwi wamshtaki Rais

Muktasari:

Ousman Sowe, Lamin Ceesay na Fatou Jatta walikuwa miongoni mwa raia wa mwanzo wa Gambia kujiunga katika programu ya matibabu dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (HIV)

 


Banjul, Gambia. Watu watatu walioathirika kutokana na tiba feki ya ugonjwa wa Ukimwi iliyobuniwa na rais wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh wamefungua mashtaka wakitaka walipwe fidia hiyo ikiwa ni kesi ya kwanza dhidi yake tangu akimbilie uhamishoni.

Waathirika hao watatu walifungua kesi katika Mahakama Kuu jijini Banjul Alhamisi, ilisema taarifa ya shirika lisilo la kiserikali la AIDS-Free World lenye makao yake Marekani ambalo linawasaidia kukusanya ushahidi.

Jammeh, ambaye utawala wake wa miaka 22 katika nchi hii ndogo ya Afrika Magharibi uligubikwa na shutuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, alikimbilia Guinea ya Ikwete mwaka jana baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu.

Ousman Sowe, Lamin Ceesay na Fatou Jatta walikuwa miongoni mwa raia wa mwanzo wa Gambia kujiunga katika programu ya matibabu dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (HIV) na Ukimwi (AIDS) mwaka 2007 ambapo walitakiwa kuacha kutumia dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo badala yake wanywe dawa ya maji iliyotengenezwa nchini ambayo iliwasababisha kutapika.

 Afya za waathirika

Afya zao zilizidi kuzorota wakati wengine waliokuwa kwenye programu hiyo walifariki dunia.

“Naamini ni wajibu wangu kumwajibisha Jammeh,” alisema Sowe, mhadhiri wa zamani wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 60 hivi.

“Nilijua kwamba siku moja ukweli utafahamika.”

Waathirika hao walisema watu walikuwa wanaogopa kumkosoa rais alipokuwa madarakani na madaktari na wagonjwa walitangaza hadharani kwamba dawa ilikuwa inafanya kazi.

Programu ile ilizorotesha mapambano dhidi ya HIV/AIDS katika nchi ambayo inashika mkia ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika katika viwango vya utoaji tiba