Wabunge kumjaza mamilioni Mwakinyo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpongeza Bondia Hassan Mwakinyo bingwa wa WBO aliyetembelea bungeni leo,kushoto ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini ,Aishi Hiraly.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Wabunge leo Ijumaa Septemba 14, 2018 wamekubaliana  kutoa Sh20,000 kila mmoja kumchangia bondia Hassan Mwakinyo

Dodoma.  Wabunge zaidi ya 300 leo Ijumaa Septemba 14, 2018 wamekubaliana  kutoa Sh20,000 kila mmoja kumchangia bondia Hassan Mwakinyo.

Mwakinyo  aliyeweka rekodi iliyoshitua dunia kwa kumchapa kwa Technical Knock Out (TKO) bondia namba nane kwa ubora duniani, Sam Eggington, ametembelea bungeni leo ambako ombi la kumchangia limeridhiwa na Spika Job Ndugai.

Juni 26, 2018 wabunge zaidi ya 300 waliwachangia Jivunie Mbunda  ambaye ni mlemavu na Bahati Ramadhan Sh20,000 ikiwa ni zawadi kwa wanandoa hao waliofunga ndoa Mei 12. Wawili hao walichangiwa fedha hizo baada ya kutembelea bungeni na kukaribishwa kwa vifijo.

Ila leo ni zamu ya Mwakinyo ambaye alimchapa Eggington katika raundi ya pili ya pambano la raundi 10 la uzito wa super welter, lililoacha mshituko kwa mashabiki wa ngumi nchini Uingereza Jumamosi iliyopita, Septemba 8, 2018.

Mara baada ya Mwakinyo kutambulishwa na Ndugai, wabunge walianza kumshangilia kwa nguvu huku wakipiga meza na makofi.

“Tunakupongeza  na tunaona fahari kuwa mwenzetu na umeliletea Taifa heshima kubwa,” amesema Ndugai.

"Ni matarajio yetu sasa hivi utasonga mbele, mbele zaidi na naomba tutakapomaliza hapa Mwakinyo apelekwe kuonana na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) popote alipo.”

Huku akicheka kuashiria kuwa ni utani Ndugai amesema, “sikujua kama Tanga mtatoa bondia. Nilijua bondia atatoka usukumani, kwa wanyamwezi wabeba mizigo mizito kumbe hakuna chochote.”

Baada ya kauli hiyo ya Spika, mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aesh Hilaly aliomba mwongozo, “tumekuwa tukiwachangangia ma-miss  humu ndani, tunaomba mwongozo wako sisi  kama wabunge tumchangie hata Sh20,000.”

Baada ya kauli hiyo ya Aeshi wabunge walipiga makofi na Ndugai kubainisha kuwa makofi hayo yameashiria kuwa wameafiki jambo hilo.