Wabunge wachanga Sh43 milioni kwa matibabu ya Lissu

Muktasari:

  • Nusu ya posho ya wabunge itatumika kuchangia gharama za matibabu ya Lissu.

Dodoma. Wabunge wamekubali kuchangia nusu ya posho yao kwa siku moja kuchangia matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Aga Khan mjini Nairobi, Kenya.

Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwaomba kuchangia fedha hizo na wabunge wakapiga makofi kuashiria kukubali.

Hakuna kiwango kamili kilichotangazwa kama malipo ya wabunge kwa siku ambayo yameainishwa kwa uwazi lakini baadhi ya wabunge wanataja kuwa posho ya kikao ni Sh220,000 hivyo nusu yake ni Sh110,000 hivyo kuwezesha kukusanywa zaidi ya Sh43 milioni.

Lissu alishambuliwa jana Alhamisi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.

Spika Ndugai akizungumzia safari ya Lissu Nairobi amesema lilikuwa ni ombi maalumu kutoka kwa wanafamilia na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Spika Ndugai amewaomba wabunge na Watanzania kutulia na kuendelea kumuombea Lissu badala ya kuendelea kulaumiana kupitia mitandao ya kijamii.

Amsema tukio hilo ni la kwanza na la aina yake kutokea tangu Bunge lilipohamia Dodoma na hasa katika kipindi ambacho Bunge linaendelea na vikao.