Wabunge waeleza wanachokitarajia bajeti ya Ofisi ya Rais

Muktasari:

  • Wabunge wamesema wanatarajia hotuba itakayojielekeza kutatua changamoto za utawala bora, utumishi wa umma na zinazoikabili Tamisemi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Wakati mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2018/19 ukitarajiwa kuhitimishwa kesho ili Bunge lianze kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, baadhi ya wabunge wameeleza wanachotarajia.

Wabunge wamesema wanatarajia hotuba itakayojielekeza kutatua changamoto za utawala bora, utumishi wa umma na zinazoikabili Tamisemi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hotuba ya ofisi ya Waziri Mkuu itahitimishwa huku hoja kadhaa zilizotikisa zikiwa ni demokrasia, kufutwa kwa vyama vya siasa, utekelezaji wa operesheni ya uvuvi haramu, matukio ya mauaji na utekaji.

Kabla ya mjadala wa hotuba hiyo kuhitimishwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri ambao wizara zao zimegushwa na hoja hizo watatoa majibu.

Ratiba ya mkutano wa 11 wa Bunge inaonyesha kuwa Ofisi ya Rais itawasilisha hotuba ya bajeti keshokutwa. Ofisi hiyo inajumuisha Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na ya Utawala Bora na Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Mjadala huo utafanyika kwa siku nne.

Mjadala huo utafanyika kukiwa na kumbukumbu ya Machi 27, Rais John Magufuli alipowasimamisha kazi wakurugenzi watendaji wa halmashauri mbili ambazo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2016/17 imeonyesha zimepata hati chafu.

Akizungumzia hotuba ya ofisi ya Rais, mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa alisema kimsingi Tamisemi imebeba nchi.

“Tunatarajia bajeti ya Tamisemi itaongezwa ili kutatua changamoto zilizopo,” alisema.

Mchengerwa ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria alisema wanatarajia Serikali itaongeza fedha kugharimia miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa nyumba za walimu, vituo vya afya, madarasa na miundombinu ya mawasiliano na usafiri.

Mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga alisema miongoni mwa mambo yatakayoibua mjadala ni kutotekelezwa kwa miradi ya maendeleo kunakotokana na fedha zilizotengwa kutopelekwa kama Bunge lilivyoidhinisha.

Alisema miradi ambayo haijakamilika kutokana na kutopelekewa fedha kama zilivyopangwa na Bunge ni ya maji na umeme vijijini.

Kalanga alisema Ofisi ya Rais inayosimamia utawala bora inapaswa kuwa na majibu ya mauaji, utekaji, ubambikiaji wa watu kesi, unyanyasaji na matumizi mabaya ya madaraka matukio yaliyoripotiwa nchini.