VIDEO: Wabunge watofautiana azimio la kumpongeza Magufuli

Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea akizungumza bungeni mjadala wa kupitisha azimio la bunge la kumpongeza Rais John Magufuli  kwa uamuzi wake wa kuendeleza Mji wa Dodoma na kuupa hadhi ya jiji, katika kikao cha 50 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Wabunge hao walipingana kuhusu kumpongeza au kutompongeza Rais Magufuli kwa kuupa hadhi mji wa Dodoma

 


Dodoma. Wabunge wamegawanyika wakati wa kujadili azimio la kumpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wa kuendeleza mji wa Dodoma na kuupa hadhi ya Jiji.

Azimio hilo limewasilishwa na Mbunge wa Kibakwe (CCM) George Simbachawene leo Juni 13 2018, ambaye katika azimio hilo amewaomba wabunge kuitaka Serikali kukamilisha haraka mchakato wa kuuleta bungeni muswada wa sheria ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu.

Wakichangia azimio hilo wabunge wa upinzani walipinga azimio hilo wakiitaka Serikali kuandaa kwanza mazingira ya miundombinu kabla ya kutangaza kuleta muswada huo wa Sheria.

Akichangia azimio hilo, Mbunge wa Liwale (CUF) Zuberi Kuchauka amehoji Serikali nini kinachotangulia kati ya Sheria na vigezo.

"Hatupingi Dodoma kuwa makao makuu ama jiji. Lakini ni kipi kinatangulia kati ya Sheria na vigezo vya kuwa jiji," amesema.

Mbunge wa Temeke (CUF) Abdallah Mtolea amesema kuwa azimio hilo lilipaswa kutanguliwa na maombi ya fedha kwa ajili ya uboreshaji wa mji wa Dodoma.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mariam Ditopile ameunga mkono azimio hilo na kuahidi kuwa wakazi wa Dodoma watampa ushindi mkubwa Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Suleiman Jafo amesema Serikali imetenga Sh 35 bilioni kwa jiji la Dodoma ili zitumike katika ujenzi wa miundombinu.