Wabunge wawalilia wavuvi, wataka kibano wapewe waagizaji nyavu

Muktasari:

Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza alisema Serikali inazuia wavuvi kuvua samaki wadogo, hivyo imezuia nyavu zenye matundu madogo lakini katika Ziwa Victoria kuna samaki ambao kwa maumbile hawawezi kuwa wakubwa kama dagaa, furu na hata sato.

Dodoma. Ukamataji wavuvi umeibua hoja bungeni, baada ya wabunge kuhoji sababu za kutokamatwa wauzaji na waingizaji nyavu zisizoruhusiwa nchini.

Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza alisema Serikali inazuia wavuvi kuvua samaki wadogo, hivyo imezuia nyavu zenye matundu madogo lakini katika Ziwa Victoria kuna samaki ambao kwa maumbile hawawezi kuwa wakubwa kama dagaa, furu na hata sato.

Rweikiza alihoji iwapo Serikali haioni kuzuia nyavu hizo, aina hizo za samaki hazitavuliwa kamwe. Pia, alihoji kwa nini wasikamatwe wanaouza na kuingiza nyavu hizo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha alisema lengo la kupiga marufuku matumizi ya nyavu zenye matundu madogo ni kuruhusu kizazi cha samaki kisipotee. “Tunazuia nyavu kutoka nje ya nchi ambazo haziruhusiwi, hata mwaka jana tulikamata nyavu na vifaa vingi ambavyo vilitoka China, vilikamatwa bandarini na Serikali inaendelea kufuatilia,” alisema.

Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka alihoji ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya benki ya wakulima nchini ili kuhakikisha wanapata tija.

Ole Nasha alisema benki hiyo imepata Sh246 bilioni kati ya Sh800 bilioni ilizoahidi na Serikali na kwamba, zitaelekezwa katika kilimo, uvuvi na ufugaji.

Mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu alihoji iwapo Serikali haioni imefika wakati wa kuhamasisha wananchi kujenga mabwawa ya kufugia samaki ili kuwawezesha wavuvi kupata kitoweo, hivyo kuacha uvuvi haramu.

Naibu waziri alisema Serikali inawekeza katika ufugaji samaki na kwamba, kuna vituo ambavyo vinazalisha vifaranga.

Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia alihoji mkakati wa Serikali wa kuwawezesha wavuvi badala ya kila siku kuchoma nyavu zao na kuwaacha maskini.

Ole Nasha alisema katika ruzuku ya kilimo wavuvi hawakusahaulika, wametengewa fedha za mikopo.