Wadaiwa sugu kutohama mtandao

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba

Muktasari:

  • Mtumiaji wa simu atakayetaka kuhama mtandao bila kubadili namba yake, atatakiwa kumaliza salio la muda wa maongezi ikiwamo kutoa fedha.
  • Sambamba na hilo, hataweza kuhama iwapo ana deni lolote, mfano muda wa maongezi. Pia,  hataweza kuhama kama namba imefungiwa au kusimamishiwa huduma.
  • Hata hivyo, mtumiaji akihama mtandao mmoja kwenda mwingine anatakiwa kusubiri kwa siku 30, kabla ya kuhama tena.

Dar es Salaam. Mfumo unaosubiriwa na wateja wa mawasiliano ya simu wa kuruhusiwa kuhama mtandao bila kubadili namba, unaonekana kuwa na masharti magumu huku ukiwabana watumiaji wanaodaiwa.

Mtumiaji wa simu atakayetaka kuhama mtandao bila kubadili namba yake, atatakiwa kumaliza salio la muda wa maongezi ikiwamo kutoa fedha.

Sambamba na hilo, hataweza kuhama iwapo ana deni lolote, mfano muda wa maongezi. Pia,  hataweza kuhama kama namba imefungiwa au kusimamishiwa huduma.

Hata hivyo, mtumiaji akihama mtandao mmoja kwenda mwingine anatakiwa kusubiri kwa siku 30, kabla ya kuhama tena.

Tanzania itaanza kutumia rasmi huduma ya kuhama mtandao bila kubadili namba ya simu ya kiganjani (MNP) Machi Mosi. Huduma hiyo tayari inatumiwa na nchi za Kenya, Morocco, Afrika Kusini, Misri, Sudan, Ghana, Nigeria na Senegal.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa mpango wa elimu kwa umma kuhusu mpango wa MNP, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba alisema lengo la mpango huo ni kuwapa uhuru wateja kutumia mtandao ulio bora zaidi, sambamba na kuongeza ushindani kwa watoa huduma.