Friday, April 21, 2017

Wadau wamsifu JPM ajira za madaktari, wamtaka aongezeRais John Magufuli 

Rais John Magufuli  

By Cledo Michael, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais John Magufuli kuagiza Wizara ya Afya iajiri madaktari 258 umeungwa mkono na wadau wa sekta hiyo wakisema utasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa matabibu hao.

Wakizungumzia uamuzi huo, wadau hao walisema hatua hiyo itafungua fursa kwa wengine wasio na ajira.

Tanzania ina upungufu wa madaktari 2,430.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), daktari mmoja anatakiwa kuhudumia watu 8,000, lakini kwa daktari mmoja nchini anahudumia wagonjwa 28,000.

Rais wa TMA, DK Nyongole alisema katika idadi hiyo ndogo ya madaktari watakaoajiriwa, ni muhimu kuyapa kipaumbele maeneo yenye uhitaji mkubwa hasa vijijini.

“Katika ajira hizi chache zilizopatikana, upangaji wake uzingatie maeneo yenye uhaba mkubwa ikiwamo mikoa ya pembezoni mwa nchi ambako hata idadi ya vifo vya akina mama na watoto ni vingi,”alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Rose Shayo alisema kuwa pamoja na idadi ya wanaoajiriwa ni ndogo, lakini hatua hiyo imetoa fursa kwa madaktari hao na kutaka wengine waongezwe.

“Mahitaji bado yapo, lakini suala muhimu ni kuliwekea kipaumbele na hela itapatikana,” alisema na kuongeza “Kama aliweza (Magufuli) kusimamia upatikanaji wa madawati na mabweni ya wanafunzi (Udsm) na hili linawezekana,” alisema Dk Shayo.

Pia, alisema endapo nchi itakuwa na wasomi wengi wasio na ajira ni jambo la kukatisha tamaa hivyo ni muhimu kutafuta namna bora ya kuwaajiri.

Mkuu wa Idara ya Uchumi wa Udsm, Dk Jehovanes Aikaeli aliungana na hoja hiyo kuwa Serikali ina uwezo wa kumudu gharama za malipo kwa kuwa idadi hiyo si kubwa.

“Hawa watu wamesoma kwa hela za Watanzania na wanapobaki nyumbani bila kazi ni hasara kubwa,” alisema na kuongeza:

“Nchi iliyo na watu wasio na ajira ni vigumu kuinuka, sekta muhimu kama afya na elimu ziendelee kutoa ajira,” alisema Dk Aikaeli.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sikika, Irenei Kiria alisema hadi kufikia Machi mwaka huu ni asilimia 40 tu ya bajeti ya afya ndiyo iliyotolewa na Serikali.

“Serikali iboreshe sekta binafsi kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya na kutekeleza sera ya upatikanaji wa bima kwa kila Mtanzania ili aweze kumudu gharama za matibabu,” alisema.

Takwimu zilizowahi kutolewa na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Obadia Nyongole kuhusu upungufu wa wataalamu hao nchini zilinukuu ripoti ya Task Force Sharing Policy Guidelines for Health Sector Services in Tanzania ya mwaka 2016, iliyoeleza kuna upungufu wa madaktari takriban 2,430, sawa na asilimia 75.

Dk Nyongole alisema kwa mujibu wa takwimu hizo vituo vya afya nchini vina mahitaji ya madaktari 771 wakati waliopo ni 57.

Alisema hospitali za wilaya zina mahitaji ya madaktari 1,760 wakati waliopo ni 441 huku hospitali za mikoa zina mahitaji ya madaktari 725 na waliopo ni 328.

Juzi, Rais Magufuli alitoa agizo la kuwataka madaktari wote 258 waliokuwa wameomba kwenda kufanya kazi nchini Kenya na kukidhi vigezo kuajiriwa hapa nchini.

Kenya iliiomba Serikali madaktari 500 ambao wangeajiriwa kwa mkataba wa miaka miwili na walijitokeza 496, lakini waliokidhi vigezo walikuwa 258. Hata hivyo, mahakama nchini humo iliweka zuio.

Uamuzi wa madaktari hao kuajiriwa nchini ulielezwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwamba alipigiwa simu na Rais Magufuli akimpa agizo hilo, huku waziri huyo akisema hajui fedha za kuwalipa madaktari hao zitatoka wapi.     

-->