Friday, November 17, 2017

Waitisha kikao kujadili ‘wachawi’

 

By Daniel Makaka, Mwananchi dmakaka@mwananchi.co.tz

Buchosa. Siku moja baada ya walimu saba wa Shule ya Msingi Soswa kujikuta wamelala nje huku wawili kati yao wakiwa wamenyolewa nywele sehemu mbalimbali za miili, uongozi wa Kisiwa cha Soswa umeitisha mkutano wa dharura wa hadhara kujadili tukio hilo.

Akizungumza na gazeti hili jana, mtendaji wa Kijiji cha Soswa, Rafael Majura alisema mkutano huo utafanyika leo katika kisiwa hicho na utahudhuriwa na wazee maarufu na viongozi wa Kata ya Bulyaheke, lengo ni kujadili namna ya kukabiliana na tukio hilo ambalo limewaletea taswira mbaya kwenye jamii na Taifa. “Tunategemea mkutano huo wa hadhara utajadili tukio hili ambalo limechafua taswira ya kisiwa hiki na kuleta hofu miongoni mwa walimu,” alisema Majura.

Majura alisema tayari viongozi wa kata wakiongozwa na mtendaji, Musa Mwilomba wamefika kwa ajili ya kikao hicho.

Naye mkazi wa kisiwa hicho, Majura Magafu alisema kitendo hicho kimeleta aibu kubwa na kwamba, lazima waliohusika wapatikane na waadhibiwe.

Akizungumzia walimu waliolazwa, mganga wa Kituo cha Afya Mwangika, Ernest Chacha alisema walimu waliokuwa wanapatiwa matibabu kituoni hapo wanaendelea vizuri.

Asimulia mkasa

Akisimulia mkasa huo, mwalimu Petro Lukas alisema walilala ndani ya nyumba zao lakini asubuhi walijikuta wapo nje na walipoingia ndani, walikuta damu zimetapakaa vyumbani na sebuleni.

Pia, alisema walikuta vibuyu vikiwa vimevalishwa shanga nyeupe vikiwa vitandani na chini, hali iliyozusha hofu na kuanza kuomba msaada kwa jamii inayowazunguka.

Lukas alisema walimu wawili wameathirika zaidi na tukio hilo kutokana na mshtuko waliopata, hivyo kupelekwa kituo cha afya kupta matibabu.

-->