Wakazi Loliondo watoa hoja tano mahsusi

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mwishoni mwa wiki alitoa taarifa ya kumaliza mgogoro kuhusu pori tengefu la Loliondo uliodumu kwa takriban miaka 26 akisema chombo hicho kitasimamia kulinda mazalia ya wanyamapori, mapitio yao na vyanzo vya maji.

Viongozi wa vijiji na kata tarafa za Sale na Loliondo mkoani Arusha wamezungumzia hatua ya Serikali kuunda chombo maalumu kitakachosimamia eneo la Loliondo na kuibua hoja tano mahsusi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mwishoni mwa wiki alitoa taarifa ya kumaliza mgogoro kuhusu pori tengefu la Loliondo uliodumu kwa takriban miaka 26 akisema chombo hicho kitasimamia kulinda mazalia ya wanyamapori, mapitio yao na vyanzo vya maji.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari juzi kwa niaba ya viongozi wa kata na vijiji, mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Mathew Siloma alisema wananchi wa Loliondo wamejenga imani kwa Serikali na hasa katika ushirikishwaji wa kutafuta suluhisho la mgogoro huo.

Siloma alitaja mambo matano ambayo Serikali inastahili kuyatambua kwa sasa ambayo moja ni ardhi ambayo imekuwa ikiingiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na wananchi kupigwa licha ya kuwa vijiji vilisajiliwa kisheria na kutambuliwa chini ya mamlaka halali za kisheria.

Alisema suala la pili ni operesheni iliyoendeshwa Agosti kuondoa watu na mifugo, akisema ilikiuka uadilifu na haikuwa agizo rasmi la Serikali hivyo kukosa uhalali kisheria.

Jambo la tatu, kwa mujibu wa Siloma, ni kumshukuru Waziri Majaliwa kwa kutambua wananchi wa Loliondo kuwa ni wahifadhi wa jadi na kwamba hakuna mgogoro kati yao na hifadhi.

Siloma alisema jambo la nne ni kuwa utatuzi wa mgogoro huo umefanyika kwa kuwashirikisha wadau na kuweka mpango wa pamoja utakaozingatia masilahi ya kila mmoja.

Mwenyekiti huyo alisema la tano ni kuwa Serikali inapaswa kuhakikisha wananchi wa Loliondo wanashirikishwa kwa kiwango cha juu katika kufikia mfumo wa usimamizi wa eneo la ardhi ya vijiji lenye mgogoro.

Diwani wa viti maalumu (CCM) wa Halmashauri ya Ngorongoro (CCM), Tina Timan alisema wameipokea ripoti ya waziri mkuu kwa mikono miwili, lakini alitaka waliofanya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa operesheni wachukuliwe hatua za kisheria.

“Sisi wananchi wa Sare tunasema wale waliofanya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa operesheni wachukuliwe hatua kwa kuwa kuna baadhi ya watu waliumizwa kwa kupigwa,” alisema Timan.

Samwel Nangiria, ambaye ni mdau wa masuala ya uhifadhi alihoji mfumo wa uundwaji wa chombo maalumu cha kusimamia eneo la Loliondo akisema haupaswi kuingilia masuala ya ardhi za vijiji.

Waziri Mkuu Majaliwa katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake alisema Serikali imekubali mapendekezo ya kamati ya uchunguzi ya kuunda chombo maalumu kitakachosimamia eneo la Loliondo kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.

Pia, aliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae muswada wa kutunga sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalumu au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti.

“Sheria itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia masilahi ya jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na mahusiano yao na matumizi ya ardhi,” alisema Majaliwa.

Waziri mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalumu utakaowasilishwa serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.

Alisema kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili waipitie kwanza. Alisisitiza rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19.

Aliwataka mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya pori tengefu la Loliondo wafanye ziara kutembelea eneo hilo ili wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za kisekta zilizopo.

Mwisho.