Wakesha kusubiri kupatwa kwa jua

Magari ya watu waliofika kukesha kwenye kituo cha maalumu cha kuangalia kupatwa kwa jua kilicho Rujewa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Katika eneo hili ambalo awali halikuonekana kuwavutia wapita njia hata kufaa kutumika kama sehemu ya kujiburudisha kutokana na shughuli ya uchimbaji mawe na upasuaji kokoto, usiku huu watu wamejaa huku watu wakijiburudisha.

Mbarali. Umati wa watu umepiga kambi eneo la Rujewa, wakisubiri tukio la kupatwa kwa jua kipete linalotokea baadaye leo.

Katika eneo hili ambalo awali halikuonekana kuwavutia wapita njia hata kufaa kutumika kama sehemu ya kujiburudisha kutokana na shughuli ya uchimbaji mawe na upasuaji kokoto, usiku huu watu wamejaa huku watu wakijiburudisha.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia watu wakiingia na kutoka eneo hilo, ambalo wataalam wa anga wameweka mitambo yao kwa ajili ya kuratibu tukio hilo la kihistoria.

Mama lishe, wachoma nyama na wauzaji wa vinywaji vikali wapo kazini kuwahudumia watu waliofika kushuhudia tukio hilo.

“Kwa kweli tukio hili ni kukumbukwa, muda kama huu ninakuwa nyumbani lakini hawa watu  lazima wahudumiwe,” mamalishe Christina Mgaya.

Hata hivyo, uhaba wa nyumba za kulala wageni katika mji mdogo wa Rujewa umesababisha baadhi ya wageni kukosa sehemu ya kulala na kukesha eneo hilo.