Wakulima wa korosho waondolewa makato

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alisema hayo na kuongeza kuwa Serikali ilishashughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho kwa kuondoa makato yasiyokuwa na lazima ikiwamo kufuta baadhi ya ushuru.
  • Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Masasi (CCM), Rashid Chuachua ambaye alitaka kujua namna gani Serikali inavyoweza kushughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho ikiwamo kuondoa makato.

Dodoma. Serikali imeondoa makato ya Sh90 kwa kilo moja ya korosho kwa wakulima wanapouza zao hilo, Bunge lilielezwa jana.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alisema hayo na kuongeza kuwa Serikali ilishashughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho kwa kuondoa makato yasiyokuwa na lazima ikiwamo kufuta baadhi ya ushuru.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Masasi (CCM), Rashid Chuachua ambaye alitaka kujua namna gani Serikali inavyoweza kushughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho ikiwamo kuondoa makato.

“Serikali imeshughulikia na kufuta ushuru wa Sh20 kwa kilo kwa ajili ya chama kikuu cha ushirika, Sh50 za usafirishaji wa korosho, Sh10 kwa ajili ya mtunza ghala na Sh10 kwa ajili kikosi kazi cha masoko,” alisema Ole Nasha.

Naibu Waziri huyo alisema sekta ya korosho ina utaratibu maalumu wa kupanga bei kwa kutumia vigezo vinavyokubaliwa kwa pamoja na wadau wote.

Alisema ununuzi wa pembejeo za korosho hufanywa kwa pamoja na vyombo rasmi ndani ya tasnia ambayo awali ilikuwa inasimamiwa na mfuko wa maendeleo ya korosho na sasa bodi ya korosho Tanzania.

Kuhusu suala la kiwango cha elimu kwa watendaji wa ngazi za msingi ambalo liliulizwa na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alisema kiwango cha elimu si kigezo cha msingi bali kinachopaswa kwa viongozi hao ni uadilifu na uaminifu katika kujitoa kusaidia vyama hivyo.